Congo DRC: Kambi Ya Upinzani Yasusia Tarehe Ya Uchaguzi Iliyotangazwa Na Tume
Tume ya uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetangaza kwamba uchaguzi mkuu nchini humo sasa utafanyika Desemba 2018.

Hatua hiyo hata hivyo haijaufurahisha upinzani ambao unataka Rais Joseph Kabila aondoke madarakani.

Uchaguzi ulipangiwa kufanyika mwaka huu chini ya makubaliano yaliyoafikiwa mwaka jana, lakini tume ya uchaguzi imechelewa kuandaa uchaguzi.

Awali, ilikuwa imetangaza kwamba uchaguzi unaweza tu kufanyika mwaka 2019.
Lakini sasa tume hiyo imetangaza kwamba uchaguzi wa rais, wabunge na viongozi wa serikali za majimbo utafanyika mnamo 23 Desemba, 2018.


Lakini upinzani umepinga tarehe hiyo na kusema haikubaliki.
Upinzani umesisitiza kwamba ni sharti Rais Kabila aonondoke madarakani kufikia mwisho wa mwaka huu.

"Tunaikataa kalenda iliyotolewa ya uchaguzi...tunachokitaka kwa sasa hivi ni Kabila kuondoka madarakani kufikia 31 Desemba, 2017," alisema Augustin Kabuya, msemaji wa chama kikuu cha upinzani cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS).

Afisa wa tume ya uchaguzi Jean-Pierre Kalamba amesema matokeo ya muda yatatangazwa katika kipindi cha wiki moja baada ya upigaji kura kufanyika, mnamo tarehe 30 Desemba, lakini matokeo kamili yatatangazwa tarehe 9 januari, 2019.
Rais mpya anatarajiwa kuapishwa 12 Januari, 2019.
Powered by Blogger.