Marekani: Watu 26 Wauawa Na Wengine 20 Kujeruhiwa Kwa Risasi Kanisani Texas

Watu 26 wameuawa kwa kupigwa risasi na mtu mwenye silaha aliyewafyatulia risasi waumini katika kanisa moja jimbo la Texas wakati wa ibaada, maafisa wanasema.
Shambulio hilo lilitekelezwa katika kanisa la First Baptist Church katika mji wa Sutherland Springs, mji mdogo katika wilaya ya Wilson, Texas.

Mshambuliaji, ambaye anadaiwa kuuawa baada ya kutekeleza mauaji hayo, aliingia kanisani na kuanza kuwafyatulia risasi watu mida ya saa tano unusu asubuhi (17:30 GMT).

Gavana Greg Abbott amethibitisha idadi ya waliofariki na kulitaja shambulio hilo miongoni mwa  visa vibaya zaidi vya mauaji ya kutekelezwa kwa kutumia bunduki katika historia ya texas.

"Kutakuwa na majonzi na masikitiko mengi kwa wale walioathiriwa," aliambia wanahabari.

Mkuu wa idara ya usalama wa Texas Freeman Martin amesema waathiriwa walikuwa na umri wa kati ya miaka 5 na 72.

Maafisa wamesema watu zaidi ya 20 pia walijeruhiwa na wamelazwa hospitalini.
Bw Martin amesema mshukiwa ni mwanamume mzungu wa umri wa miaka 20 ambaye alikuwa amevalia mavazi meusi na fulana ya kujikinga dhidi ya risasi pamoja na kuwa na bunduki yenye uwezo mkubwa.

Alianza kufyatua risasi nje ya kanisa kabla ya kuingia ndani na kuendelea kufyatulia watu risasi.
Powered by Blogger.