Stars Yaingia Kambini Bila Ulimwengu
Kikosi cha Taifa Stars kimeanza kambi huku wachezaji wengine kutoka
kikosi cha Azam FC wakitarajiwa kuingia kambini hii leo usiku huku
kikimkosa Mshambuliaji wa Kimataifa Thomas Ulimwengu.
Afisa
Habari wa Shirikisho la Soka nchini TFF Alfred Lucas amesema, taarifa
ambazo wamezipata kutoka Sweden ni kwamba Ulimwengu kwa sasa yuko chini
ya uangalizi wa madaktari wa timu hiyo ya AFC Eskilstuna.
"Kocha alitaja kikosi cha
timu ya taifa ambacho kilitakiwa kuingia kambini hapo jana, na wachezaji
walioripoti ni kutoka Mtibwa, Ruvu Shooting, Yanga na Simba SC huku
wachezaji kutoka katika kikosi cha Azam FC wakiwa bado hawajawasili
lakini tunawatarajia kuingia kambini leo usiku," amesema.
"Tumewasiliana na Thomas
Ulimwengu na ni majeruhi na anaangaliwa kila siku hivyo tukisema tumlete
huku tutaaribu ratiba ya uangalizi wake na kwa msingi huo michezo wa
timu ya Taifa ataikosa," amesema.
Hivyo sasa Mayanga atabaki na
washambuliaji Mbwana Samatta (KRC Genk- Ubelgiji), Ibrahim Ajib (Simba
SC), Mbaraka Yusufu (Kagera Sugar) na Abdul-Rahman Mussa (Ruvu
Shooting).
Taifa Stars inatarajiwa kucheza na
Botswana Machi 25, 2017 kabla ya kuivaa Burundi Machi 28, mwaka huu
katika michezo kirafiki wakati huu wa Kalenda ya Shirikisho la Kimataifa
la Mpira wa Miguu (FIFA).