Matokeo Kidato Cha Nne: Shule Saba Zaifuta Machozi Serikali

Image result for ndalichako

Hali ya shule kongwe za Serikali nchini inazidi kuwa mbaya, baada ya matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika Novemba mwaka jana kuonesha kuwa katika shule bora zenye zaidi ya watahiniwa 40 za Serikali ni saba pekee zilizoingia katika 100 bora.

Kwa mujibu wa taarifa iliyowekwa katika tovuti ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Shule ya kwanza ya Serikali ni Kibaha Sekondari ya Pwani iliyoshika nafasi ya 16 kati ya shule 3, 280 zenye watahiniwa zaidi ya 40 ambazo watahiniwa wake walifanya mtihani huo.

Taarifa hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN),  kwa kupanga shule kuanzia ya kwanza na kuzigawa kwa rangi huku zile zenye ufaulu mzuri kuwa kwenye rangi ya kijani, ufaulu wa kati rangi ya njano na ufaulu mbaya rangi nyekundu.

Taarifa hiyo imeonesha kuwa shule nyingine za Serikali kwenye 100 bora na namba ilizoshika kwenye mabano ni Mzumbe ya Morogoro (27), Kilakala ya Morogoro (28), Shule ya Wasichana Kibosho ya Kilimanjaro (36),Shule ya Wavulana Tabora (41) na Ilboro ya Arusha (42).

Baadhi ya shule kongwe za Serikali ambazo hazijaingia katika kundi hilo ni pamoja na  shule ya wasichana Tabora Girls (113) Msalato ya Dodoma (129) na Azania ya Dar es Salaam (451).

Wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya bajeti ya mwaka 2016/17, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, alisema wizara yake imeandaa mpango wa ukarabati wa shule kongwe za sekondari nchini na kwamba katika awamu ya kwanza, shule 33 zitakarabatiwa.

Alizitaja shule zilizo kwenye mpango wa kukarabatiwa kuwa ni pamoja na Ihungo, Ilboru, Kilakala, Mwenge, Msalato, Mzumbe, Nganza, Pugu, Same, Tabora Boys na Tabora Girls.

Nyingine ni Azania, Jangwani, Kantalamba, Mpwapwa, Tosamaganga, Malangali, Milambo, Nangwa, Kibiti, Minaki, Ifakara, Songea Boys, Ndanda, Kigoma, Kibaha na shule za ufundi za Bwiru Boys, Ifunda, Iyunga, Moshi, Mtwara, Musoma na Tanga.

“Mazingira ya kufundishia na kujifunzia yana mchango mkubwa katika kuinua ubora wa elimu katika ngazi zote,” alisema Profesa Ndalichako.
Powered by Blogger.