Haya hapa majbu ya Darassa juu ya maswali 10 ambayo hajawahi kuulizwa kuhusu wimbo wake wa ‘MUZIKI’
Ukitaja wasanii ambao wamefunga na kuuanza mwaka 2017 vizuri huwezi kumuacha Rapa Darassa kwani wimbo wake wa ‘MUZIKI’ umemfanya rapa huyo kujulikana sio tu Tanzania bali Afrika Mashariki yote.

Rapa Darassa amehojiwa na Gazeti la Taifa Leo la nchini Kenya na kuulizwa maswali 10 ambayo pengine haujawahi kuyasikia popote pale akiulizwa na waandishi wa Habari na Maswali yenyewe ni kama kama ifuatavyo.

Kwa nini unajiita Darassa?

Darassa: Tulikuwa studio kukatokea changamoto nikaitatua nikapewa jina Darassa nikaona linanifaa na naweza kulitendea haki. Kuona uhalisia wa maisha ni wito ambao ninao na unanishawishi kumsukuma mtu ili tusaidiane kuepuka uzembe na kutumia akili kuboresha maisha na ndio maana nikawa Darassa.

Ulitoa wapi wazo la kutengeneza ‘Muziki’?

Darassa: Wimbo huu nilitoa hisia kwenye biti ambalo lilianzishwa na produsa Mr VS kutoka kampuni yetu ya Classic Music Group (CMG). Alipiga biti hilo nikapata mzuka nikaandika mistari kabla ya kwenda kwa produsa Abba ambaye aliongezea vitu vingine kisha tukaenda kurekodi kwa Mr T Touch.

Uliamini ngoma hiyo itavuma?

Darassa: Sikuwa na uwezo wa kuingilia mipango ya Mungu kujua nitavuma leo, jana au juzi ila ile hisia ya ndani kuwa mimi nina kitu na nakifanyia kazi na kinaweza kubadilisha fani nzima nimekuwa nayo kwa miaka mingi sana.

Nani yule anacheza na taulo kwenye video yako?

Darassa: Jamaa anayecheza na taulo anaitwa Wabogojo, ni Mtanzania aliyeishi China kwa miaka mingi na ni mwana-sarakasi. Nashukuru amekuwa shabiki wangu kama ulivyoona vitu alivyovifanya na amewahi pia kuonekana katika video za wasanii wakubwa kama vile Mr Nice.

‘Muziki’ unakaa Kama wimbo wa Kikenya
 
Darassa: Sijui kwanini unasema rap yangu inaelekea kwenye flava ya Kenya lakini mimi siogopi wala sikatai kwa ajili Kenya na Tanzania zote nyumbani. Sijisikii vibaya kuambiwa nafoka kama Mkenya, ningejisikia vibaya ningeambiwa nimeiga Mrusi maana ingekuwa nimepotea sana nyumbani.
 
Unawazungumziaje wachekeshaji wanaoigiza wimbo na video yako?
 
Darassa: Joti (mchekeshaji) video yake nimeiona na nimeipenda kwa sababu inaonyesha kiasi gani nimefanya kitu kikubwa hadi kimekuwa burudani na funzo pia kupitia kichekesho na imesambaa kote. Pia kakangu kutoka Nairobi, Eric Omondi, anafanya kitu kikubwa kuhusu ngoma ya ‘Muziki’ na nimekiheshimu sana kipaji chake. Heko kwa Joti, Eric Omondi na kila mmoja anayetambua mchango wetu kwenye sanaa.

Ulikuwa wapi kabla ya kuachia ‘Muziki’?

Darassa:  Nimekuwa kwenye fani hii kwa miaka japo nilitumia muda mwingi kuifahamu kwanza kisha ndio nikaingia uwanjani. Nilitoa wimbo wangu Sikati Tamaa na Ben Pol 2013 kisha nikatoa wimbo mwingine Nishike Mkono 2014. Nikakaa kimya kwa miaka miwili halafu nikarudi 2016 na Kama Utanipenda niliyofanya na Rich Mavoko; Heya Haye na Mr Blue; Too Much; kisha Muziki na Ben Pol.

Wabongo inasemekana mnanunua sana ‘views’ za Youtube?

Darassa: Kama unaona kabisa kazi yako haina nguvu kisha una ‘viewers’ milioni basi utakuwa unajidanganya mwenyewe. Mtu kama mimi nataka kuona nguvu ya watu inafanya kazi sio ujanjaujanja kwa hiyo hakuna chochote ninachojua kuhusu kununua watu Youtube ila najua kuwaaminisha watu kwenda Youtube kujua biashara yangu.

Tutarajie Kolabo gani kubwa?

Darassa: Mimi na wasimamizi wangu tunaamini kolabo haimaanishi sisi tunamuhitaji nani au nani anavuma kwenye soko, tunazingatia wimbo unamtaka nani. Wimbo ukimtaka mtu ambaye alitoka kwenye soko miaka kumi iliyopita, mimi nitamfuata niimbe naye na wimbo utakuwa mkali.

Nani alikushawishi uingie kwenye muziki?

Darassa: Nimesikiza muziki kwa kipindi kirefu hadi fani hii ikaniingia damuni. Nimejengwa na watu wenye maana wanaojadiliwa vizuri katika jamii nami nilitamani kuwa na heshima kama wao. Watu kama Profesa Jay, Afande Sele, Mwana FA, AY yaani watu wakubwa sana nyumbani.

Darassa Kesho anatarajia kufanya Show nchini Kenya kama mambo yakienda sawa.
Powered by Blogger.