Zinedine Zidane Aingia Majaribuni

Meneja wa klabu bingwa duniani Real Madrid Zinedine Zidane, ameingia katika majaribu ya kusaka mbinu mpya ya kukiwezesha kikosi chake kuendelea kufanya vyema kwenye michezo ya ligi kuu ya soka nchini Hispania (LA LIGA).

Zidane anakabiliwa na hali hiyo, kufuatia kuumia kwa beki wake wa pembeni kutoka nchini Brazil Marcelo pamoja na kiungo kutoka nchini Croatia Luka Modric wakati wa mchezo wa mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Malaga ambao walikubali kubamizwa mabao mawili kwa moja.

Jopo la madaktari klabuni hapo, limemthibitishia meneja huyo kutoka nchini Ufaransa kuwa, wachezaji hao hawatoweza kuendelea kucheza katika michezo kadhaa inayofuata kutokana na majeraha yanayowakabili.

Akiwa katika mkutano na waandishi wa habari, Zidane alisema kiungo Luka Modric anakabiliwa na maumivu ya nyama za paja pamoja na nyonga halikadhalika Marcelo ana tatizo la nyama za paja.

Wachezaji hao wawili wanaungana na wachezaji wengine ambao ni majeruni kama Gareth Bale, James Rodriguez, Dani Carvajal, Pepe na Fabio Coentrao. Kesho Real Madrid watacheza mchezo wa mkondo wa pili hatua ya robo fainali wa kombe la Mfalme dhidi ya Celta Vigo ambao wanaongoza kwa mabao mawili kwa moja.
Powered by Blogger.