Robert Pires Amuhoji Sanchez, Abaini Ukweli Huu


Gwiji wa klabu ya Arsenal Robert Pires, ameendelea kuongeza mashaka ya mustakabali wa mshambuliaji Alexis Sanchez ambaye hafahamu hatma yake ya kuendelea kubaki Emirates Stadium.

Pires ambaye ni sehemu ya benchi la ufundi la Arsenal, amesema bado kuna ukakasi mkubwa kuhusu mustakabali wa mshambuliaji huyo ambaye anabembelezwa kusaini mkataba mpya klabuni hapo.

Pires amesema alizungumza na Sanchez kuhusu suala hilo, lakini mshambuliaji huyo kutoka nchini Chile alimjibu hafahamu nini kitakachotokea, japo anaendelea kufurahishwa na maisha ya Arsenal kwa kucheza soka lake kama inavyotakiwa.

“Hafahamu chochote kuhusu suala la mkataba wake ambalo linaendelea kufanyiwa kazi klabuni hapa, anachotaka ni kucheza soka na kufurahia hali hiyo.

Alexis Sanchez 

“Sote tunataka kuona akisaini mkataba mpya ambao utamuwezesha kubaki klabuni hapa kwa kipindi kingine. Lakini bado ninaamini atakubali kufanya maamuzi ambayo yatakua na matokeo ya furaha kwa kila mmoja wetu, kwa sababu ni mchezaji mzuri, kwangu mimi ninamfananisha na injini ya gari. Natarajia atakubalia kusaini.

“Ninamfuatilia mazoezini kila siku. Anaonekana ni mwenye nguvu na mwenye malengo makubwa na klabu hii. Anaonyesha kupevuka kiakili na kimwili.

Mkataba wa sasa wa Alexis Sanchez, utafikia kikomo mwishoni mwa msimu wa 2017/18.

Mshambuliaji huyo mwenye umri 28, tayari ameshaifungia Arsenal mabao 17 kwa msimu huu, likiwepo bao muhimu ambalo liliinusuru klabu hiyo dhidi ya Burnley mwishoni mwa juma lililopita.
Powered by Blogger.