Picha: Hatimae Klabu Ya Chelsea Imeruhusiwa Kujenga Uwanja Mpya


Klabu ya Chelsea ya Uingereza imepewa idhini na baraza la wilaya kujenga uwanja mpya mradi ambao utagharimu £500m.

Stamford bridge
 Uwanja wa sasa wa Stamford Bridge


Uwanja huo utakuwa na uwezo wa kutoshea mashabiki 60,000. Kamati ya mpangilio wa wilaya ya Hammersmith na Fulham imeidhinisha mpango wa kubomoa uwanja wa sasa wa Stamford Bridge unaotosha mashabiki 41,000.

Miongoni mwa yaliyomo kwenye mpango mpya wa ujenzi, ni pamoja na kujengwa kwa njia ya kutumiwa na watu kutembea kutoka kituo cha reli kilicho karibu. "Tunashukuru kwamba mpango wetu umeidhinishwa," Chelsea walisema kupitia taarifa waliyoitoa kupitia kituo cha Skysports.

"Uamuzi wa kamati hiyo hata hivyo hauna maana kwamba tunaweza kuanza ujenzi mara moja. Hii ni hatua tu ya karibuni zaidi, ingawa ni hatua muhimu sana, ambayo ilikuwa ni lazima tuitimize kabla ya kazi ya ujenzi kuanza, pamoja na kupokea vibali vingine."

Meya wa London Sadiq Khan atakuwa na usemi wa mwisho kuhusu ujenzi wa uwanja huo mpya.
Ramani ya uwanja huo mpya imechorwa na wasanifu mijengo Herzog na de Meuron, ambao pia walichora uwanja wa Olimpiki wa "Birds Nest" mjini Beijing.

 Mchoro wa uwanja mpya wa Stamford Bridge uliopendekezwa
 Mchoro wa uwanja mpya wa Stamford Bridge uliopendekezwa 


Hatua ya kutolewa kwa idhini ya kujengwa kwa uwanja huo inamaanisha kwamba sasa huenda Roman Abramovich akatafuta uwanja wa muda wa kutumiwa na viongozi hao wa sasa wa Ligi ya Premia kwa karibu miaka mitatu ujenzi utakapokuwa ukiendelea.

Viwanja ambavyo wanaweza kutumia ni Twickenham na Wembley. Chelsea huenda hata hivyo wakatatizika kuupata uwanja wa Wembley kwani utatumiwa na wapinzani wao Tottenham Hotspur angalau kwa msimu wa 2017-18 wanapomalizia ujenzi wa uwanja wao wa kutoshea mashabiki 61,000.

Chelsea wanaweza bado kuendelea kutumia Stamford Bridge ujenzi ukiendelea, lakini mpango huo utakuwa ghali.

Chelsea
Mpango wa eneo ambalo uwanja mpya wa Stamford Bridge utajengwa pamoja na njia ya kutoka kituo cha treni cha Fulham Broadway 


Abramovich amekuwa akitaka sana kupanua uwanja wa Stamford Bridge kwa miaka kadha sasa bila mafanikio. Miaka kumi iliyopita Arsenal walijenga uwanja wao wa Emirates unatosha mashabiki 60,000. West Ham walihamia uwanja wao wa Olimpiki unatosha mashabiki 57,000 eneo la Stratford, London mashariki na Spurs kwa sasa wanapanua uwanja wao White Hart Lane.

Uwanja wa sasa wa Stamford Bridge unatosha mashabiki 41,663 ndio wa saba kwa ukubwa miongoni mwa viwanja vinavyotumiwa na klabu za Ligi ya Premia. Uwanja wa Old Trafford unaotumiwa na Manchester United hautoshi mashabiki 76,000.
Post a Comment
Powered by Blogger.