Makavu kwa Young D, Kuhusu Matumizi ya ‘Unga’
Kuna huyu mdogo wangu mmoja, anaitwa
David Genzi, lakini ni maarufu sana kama Young D. Ninafuatilia kazi na
mambo yake, anafanya vizuri na kama anaweza kushikilia hapo alipo,
wazungu wanasema ku-maintain, anaweza kufika mbali hasa kwa kutilia
maanani umri wake ulivyo mdogo.
Kuna wasanii wengi waliingia katika hii
fani wakiwa wadogo kiumri, mfano akina Dully Sykes, Mr Blue, Abby
Skills, Dogo Hamidu (Nyandu Tozi) kwa mifano ya wachache, lakini bahati
mbaya kwao ni kuwa waliukuta muziki ukiwa bado ni wa kupata sifa na hela
kidogo ya kula. Ndiyo, kwa umri wao wakati ule, uliwasaidia maana leo,
wale walio-maintain, Dully na Mr Blue kwa mfano, wanakutana nazo, ingawa
siyo kwa kiwango wanachostahili.
Young D anakuwa katika kundi moja na
vijana wenzake wengi, akina Young Killer, Mo Music, Harmonize, Raymond
na wenzao wa kizazi chao. Wanafanya muziki na unawalipa kama ambavyo
huyu dogo alivyofanya, aliwahi kukomboa nyumba yao iliyokuwa ikisubiri
kupigwa mnada na benki baada ya familia kukopa ili kumuuguza baba yake,
ambaye bahati mbaya alifariki dunia.
Lakini pia kwa maneno yake mwenyewe,
aliwahi kununua gari kwa pesa ya muziki, kitu ambacho hakuwahi kufikiria
kama angeweza. Kwa kijana wa Kibongo wa umri wake, unaona kabisa kuwa
ni mtu mwenye maono, mipango na malengo. Big up sana kwake.
Lakini kuna upande mmoja bwa mdogo
anakuja ndivyo sivyo. Bahati nzuri aliwahi kukiri mwenyewe kuwa ni kweli
alikuwa anabwia unga, akawaomba radhi mashabiki wake na kuahidi
kuachana na tabia hiyo ya kijinga.
Lakini majuzi, mmoja wa watu
waliomsaidia, ambaye amekuwa kama mfadhili wake, alitangaza kuachana
naye baada ya msanii huyo kurudia ‘kula unga’.
Ni habari isiyopendeza, hasa kwa kijana
mdogo kama Young D. Mimi najua anaiga, hasa baada ya kuwakuta ‘kaka
zake’ wakitumia hiyo kitu, kwa umri wake, anadhani ni starehe kama
starehe zingine anazojifunza, kama kunywa pombe labda na wanawake.
Nasisitiza zaidi kuwa huyu dogo
anaathiriwa na umri na pengine ulimbukeni. Ninaamini amekulia katika
familia ya kimasikini, anaujua msoto. Sasa ghafla leo kuwa mtu mwenye
uwezo wa kupata fedha nyingi kwa mara moja, anadhani maisha yako hivyo
siku zote.
Kwa vile ninamtakia heri, nimsihi
aachane na madawa kwa sababu inawezekana. Aache kula unga kwa vile
hautamsaidia, utamporomosha na atakuwa na maisha mabaya kuliko hata
aliyowahi kuishi kabla.
Aache ulimbukeni, watoto wajanja huiga
yaliyo mema, kama anadhani yeye ni staa mkubwa, anajidanganya. Na asije
kufikiri kununua gari ndiyo kuyapatia maisha. Gari anaweza kuliuza
dakika moja tu na kitakachobaki ikawa historia.
Ana muda mzuri wa kuwa mmoja kati ya
matajiri wakubwa Afrika kupitia muziki. Kuna starehe nyingi nzuri,
unatumia fedha na akili inazunguka kuona namna gani ya kuongeza kipato.
Asimkufuru Mungu kwa nafasi aliyompa.
Kuna vijana wenzake kwa mamilioni mtaani wanaitafuta bahati kama yake,
yeye kaipata anaanza kula unga, acha mara moja dogo.