Baada Ya Kutoa Kichapo Cha 4-2, Simba Mbioni Kuivaa Azam Fc Fainali Kombe La MapinduziHatimaye klabu ya Simba imetegua kitendawili cha timu itakayocheza na Azam katika hatua ya fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar baada ya kuwachapa mahasimu wao Yanga kwa penati 4-2 katika mchezo wa nusu fainali.
Ushindi huo wa Simba dhidi ya Yanga ni kama kuchokonoa kwenye kidonda chenye maumivu makali, maana Yanga imeingia katika dimba la Amaani leo ikiwa na majeraha ya kupigwa mabao 4-0 katika mchezo wa makundi, hali iliyopelekea watani wao wa jadi Simba wawatanie kwa jina la 4G.

 Mtanange wa Simba na Yanga


Katika mchezo huo, Yanga ilionekana kuimarika zaidi huku ikisawazisha makosa iliyofanya katika mchezo dhidi ya Azam kwa kuboresha ulinzi wa kati kwa kumpanga kiungo Said Juma Makapu ambaye alifanya kazi nzuri ya kuwalinda mabeki wake wa kati Andrew Vincent na Kelvin Yondan na kufanikiwa kuvuruga mipango ya Simba.

Mbinu nyingine ambayo Yanga imeingia nayo ni kutumia mipira mirefu kwa washambuliaji wake Saimon Msuva, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke na Amis Tambwe, lakini mabeki wa Simba Abdi Banda, Mohamed Hussein, Javier Bukungu na kamanda wao Method Mwanjale walifanya kazi kubwa ya kuwadhibiti.

Mbinu hiyo ilifanya viungo wengi wa Simba waonekane hawana athari katika eneo la katikati, na kutoonekana mara nyingi wakimiliki mpira, na kufanya Yanga watawale zaidi kipindi cha kwanza kilichomalizika kwa matokeo ya suluhu ya bila kufungana licha ya mashambuli mawili makali kwa kila upande ambayo hayakuzaa mabao.

Kipindi cha pili kila timu ilionekana kubadilika na kuonesha mchezo tofauti, huku Simba ikimiliki zaidi mpira na kushindwa kutumia nafasi takriban mbili za wazi ambapo washambuliaji wake Juma Luizio, na Kiungo Mzamiru Yasin walikosa utulivu.


Simba ilifanya mabadiliko kwa kuwatoa Shiza Kichuya, Juma Luizio na Mohamed Ibrahim na Nafasi zao kuchukuliwa na Jamal Mnyate, Laudit Mavugo na Pastory Athanas huku Yanga ikimtoa Amis Tambwe na kuingia Emmanuel Martine.

Hadi dakika 90 zinakatika, Simba 0, Yanga 0 na ndipo ilipofuata mikwaju ya penati ambapo kwa upande wa Simba, Nahodha  wake Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Daniel Agyei na Javier Bukungu walifunga mikwaju yao huku mkwaju wa Method Mwanjale ukipanguliwa na golikipa Dida wa Yanga.

Kwa upande wa Yanga, penati za Haji Mwinyi, na Dida zilipanguliwa na golikipa wa Simba Daniel Agyei, huku Saimon msuva na Thaban Kamusoko wakifunga penati zao.

 Daniel Agyei, Goli kipa wa Simba

Golikipa wa Simba aliibuka shujaa wa mchezo kwa kuokoa penati mbili huku akifunga penati yake, pia alionesha kiwango kikubwa kunyaka mikwaju kadhaa ya washambualiaji wa Yanga wakati wa mchezo likiwemo shuti la Emmanuel Martine ambaye almanusura aipatie timu yake bao dakika za mwisho, lakini Agyei alisimama imara langoni.

Huu ni mwendelezo wa Simba kuinyanyasa Yanga katika michuano hiyo, ambapo leo ni mchezo wa tano kwa timu hizo kukutana, na Simba imeshinda katika michezo minne huku Yanga ikishinda mchezo mmoja.
Mchezo wa fainali utapigwa siku ya Ijumaa Januari 13 katika dimba la Amaan
Post a Comment
Powered by Blogger.