Aitor Karanka: Tutamsajili Jese Rodriguez


Klabu ya Middlesbrough ina matumaini ya kufanikisha usajili wa mshambuliaji wa zamani wa klabu bingwa duniani (Real Madrid) Jese Rodriguez ambaye kwa sasa anaitumikia Paris St-Germain.

Middlesbrough tayari wameshawasilisha ofa ya kumsajili mshambuliaji huyo kwa mkopo wa muda mfupi, na wameshaanza mazungumzo ya kukamilisha mpango huo.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 23, alijiunga na mabingwa wa soka nchini Ufaransa (PSG), mwanzoni mwa msimu huu kwa ada ya uhamisho ya Pauni milioni 21.

“Jese ni mchezaji ambaye nimewahi kufanya nae kazi. Najua umuhimu wake,” Alisema meneja wa Boro Aitor Karanka. “Usajili wake utakua muhimu sana kwetu. Nina matumaini makubwa ya kuona mambo yakikaa sawa kabla ya dirisha kufungwa.”

Karanka pia amethibitisha kuwa katika harakati za kumsajili kiungo wa klabu ya Hull City Robert Snodgrass. Tayari uongozi wa Hull City umeshaiafiki ofa ya Middlesbrough ambayo imeainisha ada ya uhamisho ya Pauni milioni 10 ambayo itatumika katika usajili wa mchezaji huyo raia wa Scotland.

“Ni mchezaji ninae muhusudu,” Alisema Karanka. “Klabu imekua ikihangaikia mpango wa kukamilisha usajili wake. Ninatarajia kuona mambo yanakaa sawa ili tuweze kumtumia siku za karibuni.”

Wakati huo huo Karanka amethibitisha kukataliwa kwa ofa ya klabu ya Leicester City ambayo imetua Riverside Stadium na kumlenga mshambuliaji Gaston Ramirez, ambaye aliwahi kuomba kuondoka klabuni hapo.

“Inasikitisha na kukatisha tamaa, kuona mchezaji kama Ramirez akitaka kuondoka, msimu uliopita aliomba tumsajili ili atutumikie, sasa inakuwaje hii leo anataka kuondoka kinyemela”.

“Hakuna yoyote ambaye ni zaidi ya klabu hii. Na mjadala wa kupokea ofa zitakazomuhusu umeshafungwa.”
Powered by Blogger.