AFCON 2017: Asamoah Gyan Atamani Kucheza Robo Fainali


Nahodha na mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ghana Asamoah Gyan anahofia suala la kuendelea kuitumikia timu hiyo katika mchezo wa hatua ya robo fainali utakao wakutanisha na Congo DRC mwishoni mwa juma hili.

Hofu kwa mshambuliaji huyo, imeibuka kufuatia majeraha ya kiazi cha mguu aliyoyapata, wakati wa mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya Misri.


Gyan alilazimika kutolewa nje ya uwanja katika mchezo huo, kutokana na jeraha lake, na mpaka sasa madaktari wa kikosi cha Ghana wanaendelea kumpatia huduma za kitabibu.

“Bado ninahisi maumivu mpaka sasa. Sijui jeraha hili litanikabili hadi lini, ninalazimika kwenda kufanyiwa vipimo vya MRI,” Gyan alimwambia mwandishi wa BBC Sport.

“Ningependa kuwa sehemu ya kikosi cha Ghana kitakachocheza dhidi ya Congo DRC, lakini sijui mustakabali wangu mpaka sasa, inanilazimu kusubiri na kuona kama itawezekana.”

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 31, ameshaitumikia timu ya taifa ya Ghana katika michezo 99 na kufunga mabao 50, na kama ataendelea kuwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo katika fainali za Afrika za mwaka huu, huenda akafikisha mchezo wa 100 na zaidi.

Michezo ya kesho ya hatua ya robo fainali.


Burkina Faso Vs Tunisia

Senegal Vs Cameroon

Siku Ya Jumapili:


DR Congo Vs Ghana

Misri Vs Morocco
Powered by Blogger.