Man Utd, Arsenal Zatunishiana Msuli Kwa Kiungo Huyu

 Man Utd, Arsenal Zatunishiana Msuli Kwa Payet
Wakati dirisha la usajili wa majira ya baridi likitarajiwa kufunguliwa juma moja lijalo, klabu nguli za nchini England Man Utd na Arsenal zimeingia vitani kwa ajili ya kumuwinda kiungo mshambuliaji kutoka nchini Ufaransa Dimitri Payet.

Gazeti la The Daily Star limeripoti kuwa, Arsenal wapo karibu zaidi kushinda vita hiyo tofauti na kwa mahasimu wao Man Utd ambao wanaongozwa na Jose Mourinho ili kufanikisha suala la usajili wa kiungo huyo wa West Ham Utd.

Arsenal wanatajwa kuwa katika mpango mzuri wa kumsajili Payet, kutokana na ukaribu uliopo baina ya wachezaji wa Arsene Wenger na Payet ambao wengi wao wanatokeo nchini Ufaransa.

Inaaminiwa kuwa Wenger anawatumia wachezaji wake kumshawishi Payet ili akubali kujiunga na The Gunners na kuikataa Man Utd ambayo inatumia sana utaratibu wa mazungumzo baina ya viongozi na sio kwa mchezaji husika.

Hata hivyo kuna uwezekano wa Man utd wakawageuzia kibao Arsenal na kuwazidi kete kutokana na kuweka hadharani malipo ya mshahara wa pauni 220,000 kwa juma, ambao wamemtengea Payet.

Lakini pamoja na kuwepo kwa vita hiyo gazeti la The Daily Star lilifanya mazungumzo na Payet ili kujua mustakabali wake kuelekea dirisha dogo la usajili, ambalo litafunguliwa rasmi mwanzoni mwa mwezi Januari 2017.

Payet alisema: “Hali halisi ya jambo hili la usajili wangu kuhusishwa na klabu nyingine linaniathirti kwa kiasi fulani, lakini ninakabiliana nalo huku nikitambua kuwa, mimi ndio mwenye maamuzi ya mwisho. Kwa sasa ninapambana ili kuisaidia West Ham Utd kufanikisha azma ya kupata ushindi kwenye michezo inayotukabili.”

“Lakini kwa ukweli kabisa, nimeimiss sana michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya. Niliwahi kuwa na furaha kuhusu michuano hiii na imepita miaka kadhaa bila kushiriki, kwa sasa nataka ndoto yangu ipevuke tena, ili niweze kuwa sehemu ya wachezaji ambao watacheza michuano hiyo mikubwa barani Ulaya.”
Post a Comment
Powered by Blogger.