Timu ya African Lyon yawatosa wachezaji wa kigeni
Uongozi wa Benchi la Ufundi la African Lyon umesema, unasajili kwa kuangalia mapungufu yaliyojitokeza katika kipindi cha kwanza lakini hawatachukua wachezaji wa kimataifa ndani ya kikosi hicho.

Mkurugenzi wa benchi la ufundi wa African Lyon Charles Otieno amesema katika usajili wa dirisha dogo watasajili kwa kuangalia nafasi zinazohitaji maboresho ikiwa ni pamoja na upande wa mlinda mlango huku wakiangalia zaidi wachezaji wa ndani kwani wanaamini wachezaji wa ndani wanavipaji na watasaidia timu katika mzunguko wa pili wa Ligi.

Otieno amesema, wameamua kutosajili wachezaji wa kimataifa kwani wameshajifunza kwa kilichowatokea kwa wachezaji watatu waliokuwa nao ambao ni William Otong, Hood Mayanja na Tito Okello ambao hawakuonekana kambini katika maandalizi ya kumalizia mchezo wa mwisho wa kufunga mzunguko wa kwanza wa Ligi na mpaka muda huu hawajui wachezaji hao walipo.

Otieno amesema, wameshafanya mazungumzo na baadhi ya wachezaji na wiki ijayo wataweza kuwataja mara baada ya kumalizana nao huku wakiangalia pia sehemu ya walinda lango la klabu hiyo kwani bado kipa wao Mcameroon Youthe Rostand yupo ndani ya klabu hiyo lakini zipo timu ambazo zinamuhitaji.

Dirisha dogo la usajili limefunguliwa hii leo kwa vilabu vyote shiriki vya Ligi na linatarajiwa kufungwa Desemba 15 mwaka huu kabla ya kuanza kwa Ligi kuu ambayo inatarajiwa kuanza Desemba 17 mwaka huu.
Post a Comment
Powered by Blogger.