Majaaliwa ya Soka la Thomas Ulimwengu njia panda.


Msakata kabumbu nyota wa Tanzania, Thomas Ulimwengu, amejikuta akiwa njiapanda juu ya majaliwa yake katika soka, baada ya kumaliza mkataba wake katika kikosi cha TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Baada ya kumalizana na TP Mazembe, mkali huyo alianza mchakato wa kwenda Ulaya kucheza soka la kulipwa, huku Yanga nao walionyesha nia ya kumsajili kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili.
Wakati ikisemekana Yanga kuwa katika mipango hiyo, klabu ya Athletic FC United (AFC) ya mjini Stockholm, nchini Sweden ambayo ndiyo iliyomuuza Ulimwengu TP Mazembe, imemtaka kuhakikisha anatua huko Januari mwakani, tayari kuitumikia timu hiyo iliyopanda daraja hadi Ligi Kuu msimu huu.

Wakati hali ikiwa hivyo, imeelezwa kuwa, Ulimwengu anatamani kukipiga Ligi Kuu Tanzania Bara kwa miezi sita ili kukilinda kiwango chake kabla ya kutimkia Ulaya, kitendo kilichowavutia Yanga na kuanza kumpigia hesabu.
Lakini kwa mujibu wa mmiliki wa AFC ya Sweden, Alex Ryssholm, Ulimwengu anatakiwa kuwasili Stockholm Januari na iwapo atashindwa kufanya hivyo, atakuwa amepoteza bahati yake.
“Milango ipo wazi (kwa Ulimwengu) kuja kuungana na wenzake Januari mwakani, hatuna tatizo naye,” alisema kiongozi huyo, alipozungumza na BINGWA hivi karibuni.
Wakala wa mchezaji huyo, Phillip Nyuki, ndiye aliyempeleka Ulimwengu katika kituo cha soka cha Alliance Academy nchini Sweden na baadaye kumuuza TP Mazembe.
Imeelezwa kuwa katika mkataba wake atakaoingia na AFC United, kutakuwa na kipengele kitakachomwezesha Ulimwengu kutua Ulaya wakati wowote itakapobidi kufanya hivyo, ukizingatia kuwa katika ligi ya Sweden, hakuna ushindani wa kutafuta timu kwenye ligi kubwa kama England, tofauti na ilivyo kwa Ufaransa kulikosheheni vipaji vya hali ya juu vya soka.
Post a Comment
Powered by Blogger.