Machache ya kufahamu kuhusu mechi ya Simba Dhidi ya Stand United.Waliodhani kwamba Simba inasimamishwa na Stand United katika mbio za kusaka ubingwa jana wote walilala mapema tu baada ya wekundu hao wa Msimbazi kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wapiga debe hao wa mjini Shinyanga.

Stand ilikuwa na rekodi ya kutofungwa kwenye uwanja wake wa nyumbani huku ikiwa imewaadhiri mabingwa watetezi Yanga na makamu wake, Azam kwa kuzichapa bao 1-0 kila moja.

Simba imevunja mwiko wa kutofungwa kwa Stand msimu huu kwenye uwanja huo wa CCM Kambarage, kwa bao safi la mkwaju wa penalti lililofungwa na mshambuliaji wake mahiri ambaye pia anaongoza katika orodha ya ufungaji wa mabao, Shiza Kichuya.

Kwa ushindi huo Simba imeendelea kujichimbia kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Soka ya Vodacom, Tanzania Bara, ikiwa na pointi 35, ikiwa ni pointi nane mbele ya mahasimu wao wa jadi, Yanga.

Pointi hizo ni sawa na wastani wa mechi tatu, jambo ambalo linaiweka pazuri zaidi Simba dhidi ya Yanga ambayo ilipoteza jana katika mchezo wake dhidi ya Mbeya City.

Katika mchezo wa jana, Kichuya alikwamisha mpira kimiani dakika ya 32 baada ya mabeki wa Stand United kumchezea rafu Laudit Mavugo eneo la hatari.

Timu zote zilionekana kucheza kwa tahadhari zikisomana mbinu, lakini Simba walikuwa wa kwanza kufika katika lango la Stand United dakika ya tatu.

Simba walifanya shambulizi zuri dakika ya 15 na kupata kona iliyochongwa na Kichuya, lakini iliishia mikononi mwa kipa wa Stand, Frank Muhonge.

Stand United walijibu mapigo baada ya kufanya shambulizi langoni mwa Simba dakika ya 18, lakini Jacob Massawe, alishindwa kufunga baada ya kupaisha shuti lake.

Katika kipindi cha pili, Mavugo alikosa bao dakika ya 47 baada ya kupiga shuti na kugonga mwamba na kurudi uwanjani.

Baadaye Simba walipoteza nafasi nyingine ya kufunga baada ya Mohamed Ibrahim kushindwa kufunga dakika ya 64 kufuatia pasi ya Kichuya.

Stand United: Frank Muhonge, Aron Lulambo, Adeyum Saleh, Erick Mlilo, Ibrahim Job, Jacob Massawe, Pastory Athanas, Seleman Kassim, Kelvin Sabato, Frank Hamis na Amri Hamis.

Simba: Vicent Angban, Janvier Bokungu, Mohamed Hussein, Juuko Murshid, Method Mwanjale, Jonas Mkude, Shiza Ramadhan ‘Kichuya’, Mzamiru Yassin, Laudit Mavugo, Mohamed Ibrahim na Mwinyi Kazimoto.

Mechi nyingine iliyochezwa kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea, wenyeji waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Ruvu.

Kutoka Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Ndanda iliichapa Tanzania Prisons bao 1-0, wakati Ruvu Shooting wakichomoza na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya African Lyon kwenye Uwanja wa Mabatini.

Azam walipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Toto Africans kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Post a Comment
Powered by Blogger.