Bodi ya Pamba sasa kuhamia mkoani Mwanza Novemba 10
Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi imejipanga kuhamishia Bodi ya Pamba katika Mkoa wa Mwanza kabla ya Novemba 10 mwaka huu ili kuhakikisha wakulima wa pamba waliopo katika mkoa huo wanapata huduma zilizo bora kwa ukaribu na haraka.Hayo yamesemwa leo mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. William Ole Nasha alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Bukombe Mhe. Doto Biteko lililohoji juu ya hatua ya serikali kwa wakulima walioathirika na pembejeo zilizotolewa ambazo hazikuwa na ubora pamoja na kuhamishia Bodi ya Pamba katika mkoa huo.

Kwa upande wa matatizo ya pembejeo, Mhe. Ole Nasha amesema kuwa serikali tayari ina taarifa kuhusu tatizo lililowapata wakulima wa pamba katika maeneo mbalimbali kwa kusambaziwa viuatilifu pamoja na mbegu ambazo hazikuwa na ubora unaotakiwa hivyo kuathiri wakulima nchini.

Naibu Waziri huyo amefafanua kuwa kufuatia changamoto hizo za uotaji wa mbegu, serikali iliamua kufanya majaribio ya utoaji wa mbegu ambazo zilikuwa zikisambazwa hapo awali bila kujua ufanisi katika uotaji wake.
Post a Comment
Powered by Blogger.