Waziri Nape Nauye awasilisha mswada wa sheriaWaziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye amewasilisha mbele ya kamati ya kudumu ya bunge ya huduma na maendeleo ya jamii, muswada wa sheria huduma za habari wa mwaka 2016

Akiwasilisha muswada huo, Nape amewataka wanataaluma ya habari kufuata weledi na maadili ya fani hiyo kwa kuepuka uchochezi unaoweza kuligharimu taifa.

Waziri Nnauye amesema Sheria hii italeta mifumo ya kisasa ya usimamizi wa sekta ya habari na mifumo ambayo inaweza kugusa au kubadili namna wanahabari walivyozoea kutenda au kufikirika kwa sasa lakini akasema sekta hiyo iwe tayari kwa mabadiliko.

“Niwaombe wanatasnia wenzangu tuwe tayari kwa mabadiliko haya ili taaluma yetu iheshimike na sisi wenyewe tuheshimike zaidi” alisisitiza Mhe. Nnauye.

Aidha Mhe. Nnauye ametoa wito kwa wadau wote kuunga mkono muswada huo utakaojadiliwa katika Bunge lijalo la Novemba mwaka huu.

“Tuko hapa kuboresha na sio kusuguana tukae tuiandae tasnia bora zaidi kwa kupitia na kutoa maoni juu ya Muswaada huu wa Sheria ya Huduma za Habari 2016” alifafanua Mhe. Nnauye.

Ameongeza kuwa kwa sasa hadi wakati wa Bunge lijalo Serikali ipo tayari kupokea na kuyafanyia kazi maboresho yatakayolenga kufikia maono ya muswada huu kutoka kwa wadau ili kuipa heshima stahiki sekta ya habari.

Alisema kuwa muswada huo licha ya huu utatatua changamoto za kutotambulika kwa sekta ya habari kama taaluma kamili inayopaswa kuheshimiwa, pia utatatua changamoto ya kukosekana vyombo madhubuti na huru vya usimamizi wa tasnia.

Alisema kutokana na hayo muswada unapendekeza kuundwa kwa Bodi ya Ithibati itakayoainisha sifa za mwanahabari na kuwasajili.

Aliitaja taasisi nyingine inayoundwa kuwa ni Baraza Huru la Wanahabari ambalo litakuwa na wajibu wa kuandaa na kusimamia maadili ya wanahabari na watawajibishana wenyewe kwa wenyewe.
Post a Comment
Powered by Blogger.