Watoto wenye Matatizo ya Moyo Kufanyiwa Upasuaji Bure na Madaktari 14 kutoka nje
Mkurugenzi wa kiwanda cha magodoro cha Dodoma Asili Bw. Haidary Gulamali amesema atawaleta madaktari bingwa 14 kuja kufanya upasuaji wa moyo bure kwa watoto watakaobainika kuwa na matatizo hayo.

Amesema madaktari hao ambao wanatarajia kuingia nchini hivi karibuni wataanzia kutoa huduma hiyo katika hospitali ya Rufaa ya Bugando mkoani Mwanza na kisha hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma.


Bw. Gulamali ametoa kauli hiyo leo (Jumapili, Oktoba 2, 2016) wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipotembelea kiwanda hicho akiwa kwenye ziara ya kukagua maeneo ya kutolea huduma za jamii mjini Dodoma.


“Mtoto wangu amefanyiwa upasuaji wa moyo mara sita na Desemba atafanyiwa upasuaji mwingine nchini India. Nikiwa nchini India nimefahamiana na kujenga urafiki na madaktari wengi wa moyo kati yao 14 watakuja nchini na kutoa huduma ya matibabu hayo bure,” amesema.


Mbali na kupeleka madaktari hao katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, pia Bw. Gulamali ameahidi kumkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Jordan Rugimbana magodoro mapya kwenye hospitali hiyo.


Wakati huo huo Bw. Gulamali amemkabidhi Waziri Mkuu magodoro 200 yenye thamani ya sh. milioni 10 kusaidia wananchi waliathirika na tetemeko la ardhi lililotokea Septemba 10, 2016 na kusababisha vifo vya watu 17 wengine 440 walijeruhiwa.


Waziri Mkuu alishukuru Bw. Gulamali kwa msaada huo na kuahidi kuwa Serikali itahakikisha magodoro hayo inayafikisha Kagera kwa walengwa kama ilivyokusudiwa.


Bw. Gulamali alisema anatarajia kuwekeza katika ujenzi wa mradi wa kiwanda cha kusindika mafuta ya alizeti kitakachogharimu sh. bilioni nne hivyo kitaongeza fursa ya ajira kwa Watanzania.
Post a Comment
Powered by Blogger.