Utofauti uliopo Kati ya Simba ya msimu uliopita na msimu huu..
Wekundu wa Msimbazi, Simba wanathibitisha kuwa msimu huu wamesajili kikosi kipana kilichosheheni nyota kadhaa baada ya juzi kuibuka Mohammed Ibrahim na kuwa shujaa wa timu hiyo kwenye pambano lao dhidi ya Mwadui FC.

Ibrahim aliyesajiliwa kutoka Mtibwa Sugar kwenye mchezo huo walioibuka na ushindi wa mabao 3-0, alionyesha kiwango cha hali ya juu na kufunga mabao mawili huku akisaidia bao la tatu alilofunga Shiza Kichuya.

Mashabiki wengi wakiwa na mawazo ya Kichuya, Laudit Mavugo na Fredrick Blagnon, Mo alithibitisha kikosi hicho msimu huu mtu yeyote anaweza kufunga.

Simba ambao wana pointi 32 wakiongoza kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, ubora wa kikosi chao unawafanya kuendelea kufanya vema kwenye michezo mbalimbali.

Awali alianza Mavugo kuzifumania nyavu na watu wote wakahamishia macho yao kwa straika huyo wa Burundi, lakini baadaye aliibuka Kichuya anayeongoza kwenye msimamo wa wafungaji kwa mabao manane.

Ukiacha Kichuya na Mavugo, aliibuka kiungo Muzamir Yassin mwenye mabao manne kwa sasa huku straika wa Ivory Coast, Blagnon akiwa amezifumania nyavu mara moja msimu huu, straika kipenzi cha mashabiki, Ibrahim Ajib, naye amezifumania nyavu mara tatu msimu huu.

Kocha mkuu wa timu hiyo, Joseph Omog, amekuwa akionekana kutopata shida ya kutafuta wachezaji baada ya kila mmoja kumpa nafasi ya kucheza kwenye kikosi hicho.

Tofauti na misimu iliyopita Simba ilikuwa na uhaba wa wachezaji ndiyo sababu iliyopelekea kikosi hicho kushindwa kutwaa ubingwa na kuambulia nafasi ya tatu huku Yanga na Azam wakiendelea kupokezana kwenye nafasi ya kwanza na ya pili.
Post a Comment
Powered by Blogger.