Sababu ya Kocha Pep Guardiola kuwazimia wachezaji wake WiFi..


Uamuzi wa Pep Guardiola kukata mtandao wa intaneti (Wi-Fi) ndani ya uwanja wa mazoezi wa klabu yake ya Manchester City unaelezewa kuwa ni kutokana na mmoja wa wachezaji wake kukutwa na simu wakati wa mazoezi.
Guardiola aliamua kuchukua uamuzi huo akiwa na matumaini ya kuwaona wachezaji wake wakiwa na ushirikiano pindi wanapokaa pamoja kwenye akademi ya klabu hiyo kuliko kujishughulisha zaidi kwenye simu zao.
Pia kuna nguvu ndogo ya mtandao wa 3G ndani ya uwanja wa mazoezi na mshambuliaji wa klabu hiyo, Sergio Aguero, ameweka wazi kwamba jambo hilo limefanyika kutokana na kile kocha alichokiona.
“Nilikuwa nikitengeneza juisi ya machungwa na wakaniuliza (wachezaji wenzake) kama ‘intaneti’ inafanya kazi. Nikawajibu labda itakuwa ina matatizo. Nilidhani walikuwa wananitania lakini walikuwa sahihi.
“Kuna siku (Guardiola) aliingia kwenye chumba cha kukanda mwili (masaji) na akamuona mwenzangu ambaye sijui ni nani, alikuwa ametulia na simu yake, labda hakupendezwa na kitendo kile.
“Amekata mtandao. Chumba cha kubadilishia nguo, chumba cha ‘masaji’ kote hatupati intaneti. Vyumba vya juu kuna nguvu ndogo ya 3G,” alisema staa huyo.
Kambi nzima ya City ipo kwenye ari ya juu baada ya mwanzo mzuri wa msimu huu wa Ligi Kuu England chini ya kocha Guardiola ambapo walishinda michezo 10 katika michuano yote kabla ya kufungwa na Tottenham wiki iliyopita.
Guardiola anaonekana kuhitaji ushirikiano wa hali ya juu kikosini mwake na lugha anayoitumia kuwasiliana na wachezaji wake ni Kiingereza licha ya wachezaji wapya kama Nolito kupata shida ya kuing’amua lugha hiyo ngeni kwao, huku pia wakipata kifungua kinywa na chakula cha mchana pamoja.
Chakula cha usiku pia wamekuwa wakila pamoja kila baada ya mchezo wanaocheza wakiwa nyumbani dimba la Etihad, wakitumia fursa ya ukumbi mpya wa wachezaji uliojengwa majira ya kiangazi
Post a Comment
Powered by Blogger.