Miradi 1,387 yazinduliwa na Mbio za Mwenge, 2016.
Serikali imesema kuwa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2016, zimezindua jumla ya miradi 1,387 yenye thamani ya shilingi bilion 494.8 na mingine imeanza kutoa huduma kwa wananchi wa Tanzania katika kufanikisha nchi ya uchumi wa kati kupitia miradi hiyo.

Hayo yamezungumzwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama, wakati wa kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru kilichofanyika wilayani Bariadi mkoani Simiyu.

Amesema miradi hiyo ni ongezeko la asilimia 7.6 kutoka miradi iliyozinduliwa na mbio hizo mwaka jana 2015, ambapo jumla ya miradi 1,343 yenye thamani ya shilingi bilioni 463.5.

Waziri Mhagama amesema kuwa miradi mingi iliyozinduliwa imewahusisha moja kwa moja viojana kwa kuwa ndio nguvu kazi ya taifa ambayo inatarajiwa kutumika kwa ajili ya kufikia uchumi wa katika mpaka ifikapo mwaka 2025.

Aidha Waziri huyo ameongeza kuwa serikali ya awamu ya tano imesema serikali itazisimamia ipasavyo fedha zinazotolewa kwa ajili ya vijana kujikwamua kiuchumi katika halmashauri ili ziweze kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuwachuhukulia hatua wale wote watakaobainika kufanya ubadhirifu huo.

Pia ameitaja mikoa sita iliyofanya vizuri katika utekelezaji wa malengo ya mbio za mwenge ikiwa ni pamoja na matumizi sahihi ya fedha za umma kuwa ni Simiyu, Njombe, Mwanza, Ruvuma, Mbeya na Mtwara.

Kwa upande wake mgeni rasmi katika kilele cha mbio hizo za Mwenge, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Mwenge wa Uhuru ni nguzo muhimu katika kuleta maendeleo ya nchi lakini pia unadumisha amani na mshikamano baina ya watanzania wote huku ikiwaangazia zaidi vijana katika kujikwamua kiuchumi.

Kilele hicho cha mbio za Mwenge ambacho kitaifa kimefanyika Mkoani Simiyu kimeendana na maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 17 ya kifo cha muasisi na baba wa taifa katika uongozi Mwalimu Julias Kambarage Nyerere.

Katika mwaka ujao wa 2017, Mbio hizo zitazinduliwa katika mkoa wa Katavi, na kuhitishwa katika mkoa wa Mjini Magharibi, visiwani Zanzibar.
Post a Comment
Powered by Blogger.