Memphis Depay aelezea kinachomnyima raha ndani ya Mashetani wekundu...Winga mwenye wakati mgumu wa kupata namba kwenye kikosi cha kwanza cha klabu ya Manchester United, Memphis Depay, amesema kwamba hana furaha ya kubaki hapo kwani hatapewa muda wa kutosha wa kucheza.

Depay mwenye umri wa miaka 22, alijiunga na United akitokea klabu ya PSV Eindhoven katika majira ya kiangazi ya mwaka 2015, aliwahi kusema uhamisho wake ulichagizwa na ‘kocha bora wa dunia’, Louis van Gaal.

Msimu uliopita mchezaji huyo alianza kukosa namba kikosi cha kwanza na msimu huu chini ya kocha mpya, Jose Mourinho amecheza mechi tatu tu za Ligi Kuu England akitokea benchi na amesisitiza hatakuwa na sababu ya kubaki kama hali ikiendelea hivyo.

“Mimi ni yule yule na ninajua ninachokitaka,” Depay aliliambia gazeti la Uholanzi, Metro Nieuws.
“Mimi si wa kuanzia benchi. Sina furaha ya kuwa mchezaji ambaye nipo hapa kwa sababu tu ya kwamba niko chini ya mkataba na Manchester United. Hii ni klabu ya ndoto yangu lakini nahitaji kucheza.”

Licha ya kumkubali kocha wake wa zamani wa United, Van Gaal, Depay anakiri kuwa timu imeimarika chini ya Mourinho, kitu kinachofanya apate wakati mgumu wa kuanza kikosi cha kwanza.
“Mazoezi yanaendelea vizuri, niko fiti, lakini kila mchezaji yuko fiti pia,” alisema.

“Mourinho amenieleza namna anavyoniamini,hata kwenye vyombo vya habari pia.”
Ingawa Depay amekuwa akipokea lawama za kutoonesha kiwango chake baada ya kusajiliwa kwa kitita kikubwa cha fedha, alisema hahitaji msaada kutoka kwa mchezaji mwenzake yeyote na rafiki yake Paul Pogba aliyetua Old Trafford kwa gharama iliyoweka rekodi ya dunia.

“Mimi na Pogba tunajuana muda mrefu, tutashirikiana tu na si kwamba nahitaji msaada, kwani najiamini na uwezo wangu,” alisema.
Post a Comment
Powered by Blogger.