Maoni ya baadhi ya mashabiki wa klabu ya Yanga baada ya klabu kukodishwa..Wanachama wa klabu ya soka ya Yanga wametoa maoni baada ya kuona muhtasari wa mkataba ambao timu yao imeingia kuikodisha nembo yake kwa Kampuni ya Yanga Yetu Limited.

Baada ya kukubali kwa kauli moja kuikodisha nembo ya timu kwa miaka 10 wakati wa Mkutano Mkuu wa Agosti 6, 2016, Bodi ya Wadhamini ya klabu hiyo Septemba 3, 2016 ilisaini mkataba na kampuni ya Yanga Yetu Limited ambao taarifa ya muhtasari yake ilitolewa jana na kupokelewa kwa mitazamo tofauti na wanachama wa klabu hiyo.

Wakizungumza na mwakilishi wa See the Africa kwa nyakati tofauti baadhi ya wanachama wa Yanga waliweka wazi kuwa wamesoma muhtasari wa mkataba huo na kuupokea kwa furaha kutokana na ukweli kuwa wanaamini utaisaidia timu hiyo kujikwamua kiuchumi.

Sudi Hussein mwanachama mwenye namba 0000079 anayetokea tawi la Yanga, Sinza alisema jambo hilo ni la kheri kwa klabu yao kwa sababu kampuni hiyo imeonyesha kuwa inataka kuifanya timu hiyo kufika mbali zaidi kimataifa.

“Kaonyesha (Mmiliki wa Yanga Yetu Limited) amedhamiria kuipeleka Yanga kimataifa kitendo cha kutoa uwanja ni ishara tosha kuwa kwa miaka kumi ya utawala wake itakuwa na neema kwa klabu,” alisema.

Mohamed Said mwanachama wa tawi la Yanga Kariakoo alisema kitendo cha kuipa timu kampuni hiyo ni cha kheri kwa sababu imeonyesha nia ya dhati ya kuwekeza kwenye maendeleo ya klabu na kuifikisha mbali zaidi na kuifanya iwe tishio barani Afrika.

Kwa upande wake kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm, alisema kitendo cha kuikodisha nembo ya klabu kwa miaka 10 ni chenye manufaa kwa klabu hiyo na anaamini ujio wa kampuni ya Yanga Yetu Limited utainufaisha zaidi klabu hiyo na kuinyanyua zaidi Afrika.

“Ni mpango mzuri sana ambao binafsi naona utainufaisha klabu, sioni tatizo lolote kwenye hili, napenda kuwapongeza wanachama wenzangu kwa maamuzi haya mazuri,” alisema Pluijm.

Naye Katibu wa Baraza la Wazee wa klabu hiyo, Mzee Ibrahimu Akilimali, amesema hatambui mkataba huo na ataendelea na msimamo wake wa kutoutambua.

“Binafsi mimi siutambui mkataba huu, nitakutana na wazee wenzangu twende kwa mwanasheria kupata tafsiri nzuri kuhusiana na huu mkataba kisha tutatoa tamko kuna mambo mengi sana yamevunjwa kikatiba,” alisema Mzee Akilimali.
Post a Comment
Powered by Blogger.