Machache ya kufahamu kuhusu Azam FC ndani ya Shinyanga..


Timu ya Azam FC tayari iko mkoani Shinyanga ikijiandaa kuwakabili wenyeji wao Stand United katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa kesho katika Uwanja wa Kambarage, huku timu hiyo ikiwa kamili gado baada ya nyota wake kadhaa, akiwamo Pascal Wawa na Erasto Nyoni waliokuwa majeruhi kupona.
Wanalambalamba hao waliwasili Shinyanga juzi, huo ukiwa ni mchezo wao wa nne ugenini, ikiwa ni baada ya kuzifuata Mbeya City na Prisons zote za mkoani Mbeya kabla ya kutua Mtwara kukipiga na Ndanda FC.
Katika mchezo huo wa kesho, Azam watakuwa na shughuli pevu ya kupata ushindi mbele ya Stand United ambao katika michezo minane iliyopita haijapoteza hata mmoja.
Ugumu zaidi katika mtanange huo ni kutokana na Azam kukosa huduma ya beki wake mahiri wa kulia, Shomari Kapombe, anayeuguza majeraha, japo Wawa na Nyoni wameleta matumaini mapya baada ya kukosekana kwa muda mrefu.
Wanalambalamba hao wanashika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi zao 11, baada ya kushuka dimbani mara saba.
Ligi hiyo itaendelea kwa michezo mingine katika viwanja vitano tofauti ambapo kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, wenyeji wa Mkoa wa Mwanza, Mbao FC na Toto Africans zitaonyeshana kazi, huku Mwadui FC wakiwa nyumbani kuwakaribisha African Lyon.
Mjini Songea, Majimaji watakuwa wenyeji wa Kagera Sugar, huku Wanalizombe hao wakiwa na morali ya juu kupambana kupata ushindi ili kujitoa mkiani mwa ligi wakiwa wameshinda mchezo wao mmoja tu wa kwanza dhidi ya Mbao tangu kuanza kwa ligi msimu huu.
Maafande wa JKT Ruvu na wenzao wa Tanzania Prisons wanaolingana pointi, wakiwa na pointi tisa kila mmoja, wataonyeshana umwamba kwenye Uwanja wa Mabatini, mkoani Pwani katika mchezo mwingine wa ligi hiyo.
Mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Yanga, wao watashuka dimbani keshokutwa kupepetana na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, wakati Ruvu Shooting watakipiga na Ndanda Uwanja wa Mabatini.
Post a Comment
Powered by Blogger.