Kocha Salum Mayanja mbioni kurithi mikoba ya Kiweru Mwadui..


Kuna uwezekano mkubwa kocha Salum Mayanga akatua katika kikosi cha Mwadui FC ili kuchukua mikoba ya Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ aliyejiuzulu.
Julio alijiuzulu kuifundisha Mwadui  kutokana na kile alichodai kuwa kuchoshwa na uchezeshaji wa hovyo wa waamuzi katika Ligi Kuu Bara.
Habari za uhakika zilizolifikia BINGWA zinadai uongozi wa Mwadui tayari umekutana na Mayanga hivi karibuni mkoani Shinyanga.
Chanzo hicho kilidai kuwa baada ya pande hizo mbili kukutana na kuzungumza hatimaye zilikubaliana kisha kocha ambaye kwa sasa anainoa Mtibwa Sugar alirejea Dar es Salaam kwa ajili ya kuiongoza timu yake ilipoikabili Azam FC.
“Mayanga ameshakubaliana na uongozi wa Mwadui, Jumatatu alikuwepo Shinyanga kwa ajili ya mazungumzo  ambapo Jumanne alirejea Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo na Mtibwa.
“Hata hivyo, amewapa masharti viongozi wa Mwadui kutoliweka wazi suala hilo  hadi hapo atapokabidhi barua kwa uongozi wa Mtibwa kwa ajili ya kuachana nao,” kilisema chanzo hicho.
Alipoulizwa kuhusiana na suala hilo, Mayanga alikana kufanya mazungumzo na uongozi wa Mwadui na kusema yeye amesikia tu lakini hajafuatwa rasmi.
“Sijafanya mazungumzo na Mwadui, ila wao wananihitaji pia suala la kwamba nilienda kule si kweli bali nilikuwa katika msiba kijijini na leo (jana) asubuhi nimekuja Dar es Salaam kwa ajili ya  kuendelea na majukumu yangu ya kikazi,” alisema Mayanga.
Post a Comment
Powered by Blogger.