Klabu ya Zesco Yamng'ang'ania Lwandamina

Klabu ya Zesco ya Zambia imekana kocha wao George “Chicken” Lwandamina kuingia mkataba na mabingwa wa soka nchini Yanga.

Klabu hiyo ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari jana ili kuondoa uvumi uliozagaa kuwa, kocha huyo umejiunga na timu hiyo ya Tanzania kwa mkataba wa miaka miwili, wakati ana mkataba hadi Januari mwakani.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Katibu Mkuu, Richard Mulenga na Ofisa Habari Katebe Chengo, inasema kuwa, kocha huyo alikuwa na msiba na anajua nini kitatokea endapo atavunja mkabata na Zesco.

Tangu ajiunge na Zesco United ametwaa mara mbili mataji ya ligi na kuiongoza timu hiyo kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika mwaka huu.

Lwandamina ana mkataba wa miaka mitatu na Zesco United, ambao unamalizika Januari mwakani.

Klabu hiyo imesema kuwa yenyewe inachojua ni kwamba kocha wao yuko Monze katika msiba baada ya kuomba ruhusa kutoka kwa Meneja wa timu hiyo, Mabvuto Banda na alitarajia kurejea jana kwa ajili ya ratiba za katikati ya wiki watakapocheza dhidi ya Nkwazi FC mjini Lusaka leo.

Zesco United inapenda kusema kuwa endapo hayo yanayoelezwa na vyombo vya habari ni kweli, basi Lwandamina atakuwa amevunja mkataba na klabu hiyo.

Taarifa hiyo ya Zesco imetolewa na Katibu Mkuu, Richard Mulenga na Ofisa Habari Katebe Chengo.
Post a Comment
Powered by Blogger.