JPM Aonyesha Jeuri ya Pesa
Ni wazi kwamba Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli imeanza kudhihirisha kwa vitendo, kauli kwamba deni la Tanzania nje ya nchi ni himilivu baada ya kuanza kulipa sehemu ya deni ikiwa na chini ya mwaka mmoja madarakani.

Takwimu zilizotolewa mwishoni mwa wiki na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu zimebainisha hali ya uchumi kuimarika kwa kasi, hatua ambayo imewezesha serikali kuanza kulipa madeni na kutekeleza mipango mikubwa ya maendeleo.

Akithibitisha uwezo wa serikali kuanza kulipa deni la nje na la ndani ambalo limekuwa likipigiwa kelele nyingi na wabunge hususani wa kambi ya upinzani kuwa halihimiliki huku serikali ikisisitiza kuwa ni himilivu, Gavana Ndulu amesema tayari serikali imeanza kulipa madeni hayo kwa kasi.

Gavana Ndulu alisema juzi kuwa BoT imeanza kulipa madeni yote ya ndani na nje kwa fedha zake za ndani ambapo tayari imeshalipa kiasi cha Sh bilioni 96 za deni la ndani huku ikilipa dola za Kimarekani milioni 90 (sawa na Sh bilioni 190) za deni lake la nje.

Alisema kufuatia serikali kulipa Sh bilioni 96 za deni la ndani, deni hilo linasalia kiasi cha Sh trilioni 9.9 huku deni la nje linalofikia dola milioni 620 zikiwamo fedha za mkopo kutoka Benki ya Stanbic, likipunguzwa kwa dola milioni 90.

Ndulu aliwahakikishia wananchi kuwa, uchumi wa Tanzania uko imara, kukiwa na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni zinazofikia dola bilioni 4, huku ikiendelea kutumia fedha zake za ndani kuendesha shughuli za nchi bila kutumia mkopo kutoka nje, licha ya kwamba inahitajika hususani ile nafuu.

Post a Comment
Powered by Blogger.