Jose Morinho awapigia goti mashabiki wa timu ya Manchester United.


JOSE  Mourinho amewaomba radhi mashabiki wa Manchester United kutokana na kipigo cha mabao 4-0 walichokipata kutoka kwa Chelsea katika mchezo wa Ligi Kuu England, uliochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Stamford Bridge, jijini London.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mchezo huo, Mreno huyo alisema kikosi chake kilikumbana na kipigo hicho kutokana na makosa ya kijinga mno ya safu ya ulinzi.

Ni katika mchezo dhidi ya Barcelona pekee Novemba, 2010 kocha huyo alifungwa idadi kubwa ya mabao katika michuano yote na kwamba akiwa ndani ya United, matokeo hayo ni mabaya zaidi kwa Mourinho kuyavumilia.

Mourinho alisema: “Hali ilianza kuwa mbaya baada ya sekunde chache. Tulikaribia kuwa bao 1-1 na baada ya makosa ya ulinzi matokeo yalikuwa 2-1. Kutokana na mikakati tuliyokuja nayo, hatukustahili kuruhusu mabao kama ilivyokuwa.

United ilianza kuruhusu nyavu zake kutikiswa katika sekunde ya 34 pale Pedro alipopachika bao la kwanza, kabla ya mengine matatu kutoka kwa Gary Cahill, Eden Hazard na N’Golo Kante.

Mara ya mwisho United kupoteza mchezo kwa zaidi ya mabao manne ugenini ilikuwa ni dhidi ya Chelsea kwenye Uwanja wa Stamford Bridge mwaka 1999.

“Kwa maana ya pointi, tulipata sifuri, tulipoteza pointi tatu. Tupo nyuma kwa pointi sita kutoka kileleni, tatu nyuma ya mstari wa nne bora (top four), sasa tunatakiwa kushinda mechi zetu.

“Tunatakiwa kushinda mechi zetu sasa, jambo ambalo si rahisi, tunatakiwa kushinda ili kupunguza pengo la pointi, baada ya mechi hizi tatu za mwisho, tumepoteza mbili kati ya tisa, kwa sasa tunahitaji pointi.”

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 53, aliwaomba msamaha mashabiki baada ya kipigo hicho cha aina yake.

“Walitushambulia kwa dakika zote 90 katika hali ya kushangaza, mashabiki tulionao duniani kote, wapo katika hali ngumu na ninawaomba msamaha wote popote walipo,” alisema Mourinho.

“Ninapenda kuwaomba radhi kwa yaliyotokea na kitu pekee ninaweza kukisema mimi ni Man United asilimia 100 na si 99 na asilimia moja ni kwa Chelsea au klabu nyingine yoyote na kutokana na hilo, nipo katika wakati mgumu mno.

“Lakini kuna jibu moja tu, kama nilivyokuwa nikiwaambia wachezaji, kuna jibu moja tu-kujifua vilivyo kesho (jana) na kuendelea kupambana.”
Post a Comment
Powered by Blogger.