Anachokiamini Kocha Arsene Wenger kwa mchezaji Alex Oxlade-Chamberlain.
Arsene Wenger anaamini kwamba mchezaji wake, Alex Oxlade-Chamberlain, amefikisha umri ambao anajua kile kinachohitajika kwake ndani ya jezi ya Arsenal.

Winga huyo wa England alipachika mabao mawili na kuipa ‘The Gunners’ ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Reading, usiku wa kuamkia jana na kutinga robo fainali ya Kombe la EFL.

Mabao hayo yalimfanya Chamberlain afikishe mabao matano msimu huu, ikiwa ni takwimu ya kuridhisha tangu ajiunge na klabu hiyo mwaka 2011, lakini kijana huyo mwenye umri wa miaka 23 alisema hana furaha juu ya idadi ya mechi alizocheza hivi karibuni.

Chamberlain amecheza mechi nne tu za Ligi Kuu England akimaliza dakika 90 za michezo miwili tu msimu huu na kinda huyo wa zamani wa Southampton amekiri kuwa huenda akatafuta maisha sehemu nyingine kama hatapewa muda wa kutosha wa kucheza.

Lakini Wenger ambaye alifanya mabadiliko ya wachezaji tisa kwenye mchezo huo dhidi ya Reading, alisema Chamberlain amefikia hatua nzuri katika maisha yake ya kucheza soka.

“Chamberlain si kinda tena ana miaka 23, umri uliokamilika kwa mcheza soka. Kabla ya kufika miaka 23, unakuwa na muda mwingi wa kujifunza.

“Ukifika miaka hiyo, unakuwa na ukomavu, unatambua nini kinachotegemewa kutoka kwako, unajua kushughulika na presha na ushindani ndani ya kikosi.

“Chamberlain amekomaa sasa, anavyofunga mabao unaona wazi namna anavyojiamini. Hivi sasa tunapata matumaini kila anapokuwa na mpira, chochote kinaweza kutokea.

“Ni mchapakazi mazoezini, hapo anaonekana kabisa kufuata nyayo za Theo Walcott.

“Ana nafasi yake kikosi cha kwanza kwa sababu alicheza dhidi ya Ludogorets, amecheza usiku wa leo (juzi) kama ilivyotegemewa, lakini mchezo dhidi ya Ludogorets ulikuwa muhimu mno. Aliingia kwenye mchezo dhidi ya Middlesbrough wikiendi iliyopita na nadhani tayari ameshajihakikishia nafasi yake kikosini,” alisema Wenger
Post a Comment
Powered by Blogger.