Yanga - Ubingwa Ligi Kuu Matatani

 
Kocha Mkuu wa Yanga, Hans Pluijm amekiri kwa kusema kuwa kutetea ubingwa wao si kazi rahisi kwa kuwa kila timu wanayokutana nayo huwakamia kuvunja rekodi yao kimichezo.

 Pluijm alisema kutokana na kutambua hilo, ndio maana wamejiwekea malengo ya kuhakikisha wanapambana kwa kila mchezo kupata pointi tatu.

Alisema kutokana na ubora wa kila timu katika ligi, ni ngumu kuzungumzia mapema kama wataendelea kuwa mabingwa kwa msimu huu, kwani kila timu imejipanga kuonesha uwezo na hamu ya kuliwania taji.

“Laiti kama uwanja ungekuwa unazungumza nani atashinda taji msimu huu, ningetoa nafasi ya kusema, kuna ushindani mkali na kila timu imejipanga dhidi yetu kutuvua ubingwa,”alisema.

Alisema, “lengo letu tunataka kuongoza kwenye ligi ikiwezekana tuje tumalize hivyo, lakini inatubidi tusubiri tuone itakuwaje hadi mwishoni mwa msimu, unajua soka wakati mwingine haitabiriki,”alisema.
 
Pluijm alisema lolote linaweza kutokea wakati wowote na kila kitu kinawezekana na wakati mwingine huenda kisiwezekane, akiweka msisitizo kuwa anahitaji vitendo vionekane zaidi kuliko maneno.

Yanga inatarajiwa kucheza mchezo ujao dhidi ya Ndanda FC kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara, ikiwa ni mchezo wake wa kwanza wa ligi utakaochezwa nje ya Dar es Salaam.
Post a Comment
Powered by Blogger.