Makampuni Kugombania Udhamini Yanga

 
Wakati bodi ya wadhamini ya klabu ya Yanga ipo kwenye hatua za mwisho kumkodisha Yusuf Manji timu, uongozi wa Yanga leo unashindanisha wadhamini kwenye ukumbi wa Double Tree, Dar es Salaam.


Katibu Mkuu wa Yanga, Bw. Baraka Deusdetit alisema kuwa kwenye hafla hiyo itakutanisha wadau kutoka kampuni mbalimbali ambao watawasilisha zabuni zao kwa ajili ya kuingia mkataba wa kuidhamini klabu hiyo ambayo imekacha udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).

“Kuna makampuni mbali mbali ambayo yamepewa mialiko, tenda zao zitashindanishwa atakayekuwa na dau zuri ndiye tutakayeingia naye mkataba,” alisema Baraka.

Yanga imeibuka na mpya hiyo ikiwa ni wiki chache tangu ivunje mkataba na TBL kwa kile walichoita kuwa ni haramu.

Mwenyekiti wa klabu hiyo, Manji alisema kuwa mkataba wa TBL ulikuwa haramu ndio maana aliuvunja na kuingia mkataba na Kampuni ya International Marketing ambayo imepewa kazi ya kusimamia zoezi hilo kuhakikisha Yanga inapata mdhamini wa kueleweka.

“Mkataba wa kampuni ya bia nchini (TBL) na Yanga ulisainiwa miaka mitano iliyopita na mtangulizi wangu (Lyod Nchunga). Huu ulikuwa mkataba haramu,” alisema Manji katika moja ya taarifa zake kuhusu kuvunja mkataba huo. “Mamlaka ya kutia saini mikataba kwa mujibu wa Katiba ya Yanga yapo kwa wadhamini na hapana kitu kama azimio kutoka bodi ya wadhamini kuingia katika makubaliano kama haya, au mkataba kusainiwa na wadhamini,” alisema.

Alisema katika kipindi chake kilichopita alijitahidi kurekebisha tofauti zote zilizokuwepo kwenye mkataba huo, lakini alishindwa.

“TBL ni mara moja tu imetoa Sh milioni 20 kwa ajili ya tamasha la Yanga zilizoahidiwa kutolewa kila mwaka, haijailipa klabu fedha ya marekebisho inayofikia Sh milioni 30 wala haijatupa basi kwa kiwango sahihi tulichotaka kama ilivyokuwa imeahidi ndio maana tuliuvunja,” alisisitiza.

Alisema International Marketing ambayo ndio inasimamia hafla hiyo ya leo ni kampuni ambayo alikuwa Mwenyekiti wake ambayo awali ilimpitisha kuidhamini Yanga na tayari timu hiyo inavaa jezi zenye nembo ya Quality Group ambayo ameidhamini kwa Sh milioni 88. Hivi karibuni Manji alitangaza Yanga inadaiwa Sh bilioni 5.445 ambazo pia imeshindwa kuzilipa.
Post a Comment
Powered by Blogger.