Chadema Matatani, Kwa Kuhonga Vijana Pesa Kshiriki UKUTA


Jeshi la polisi Kanda ya Dar es Salaam limekituhumu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwalipa fedha kiasi cha Sh 40,000 baadhi ya vijana ili washiriki katika maandamano ya Ukuta ya Septemba Mosi yaliyopigwa marufuku.
Aidha, imesisitiza imejipanga kikamilifu kukabiliana na watu watakaovunja sheria kwa kufanya maandamano hayo ambayo yamepigwa marufuku kwa lengo la kutaka kuvuruga amani ya nchi.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Kamanda wa Kanda hiyo, Simon Sirro wakati akizungumza jijini Dar es Salaam ambapo alisema, kwa sasa jiji hilo liko shwari na hata baada ya Septemba Mosi, litaendelea kuwa shwari.

“Naomba niwasihi Wana Dar es Salaam hasa vijana wasiingie barabarani hiyo tarehe moja, tuwaachie wachache ambao nia yao ni kuleta fujo, wote tunajua madhara ya fujo, wote tunajua hasara ya fujo, siku hiyo imetolewa katazo hakuna maandamano,” alisema Sirro.

Alisema kwa taarifa za intelijensia walizonazo zinaonesha kuna watu wanapewa fedha kwa ajili ya kuandamana na kufanya fujo, ambapo alitoa rai kwa wazalendo wa nchi wasiopenda kupambana na Jeshi la Polisi ambalo linawalinda wao na mali zao wasithubutu kuingia barabarani.

Akizungumzia tuhuma hizo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji alisema, chama hicho hakina fedha za kuwalipa vijana ili kufanya maandamano na kusisitiza; “Tukutane tarehe moja Septemba.”

Julai 27, mwaka huu Chadema ilizindua operesheni iliyopewa jina la Ukuta ikiwa na lengo la kupambana na kile ilichokiita udikteta nchini, huku ikitangaza kushirikiana na wale watakaoona umuhimu wa kuwepo kwa haki na demokrasia nchini.
Post a Comment
Powered by Blogger.