Achinja Mbwa Na Mwanafunzi Wa Darasa La Tatu.
MWANAFUNZI Sarah Kisama, aliyekuwa anasoma katika shule ya msingi Nyamuswa B, darasa la tatu, iliyoko tarafa ya Chamriho wilaya ya Bunda, mkoani Mara, ameuawa kwa kukatwa kwa panga na mwanamume aliyekuwa mpangaji kwenye nyumba yao.
Inadaiwa kuwa, awali mwanaume huyo ambaye jina lake halijafahamika kutokana na kutokuwa na siku nyingi nyumbani hapo, alianza kuua mbwa kwa kumchinja kwa panga na kisha akamuweka ndani ya begi la kutunzia nguo na kulitupa ndani ya chumba kimoja cha nyumba hiyo.

Ofisa Tarafa ya Chamriho, Boniphace Maiga, alisema tukio la kuuawa kwa mwanafunzi huyo lilitokea Agosti 23, mwaka huu, saa 1:30 usiku katika nyumba anayoishi mtoto huyo iliyopo kijiji cha Makongoro B, wilayani hapa.

Maiga alisema baada ya kumuua mtoto huyo mtu huyo alitorokea kusikojulikana na kwamba sasa anatafutwa na Polisi ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria, kujibu tuhuma za mauaji.

Maiga akisimulia mkasa huo alisema mtuhumiwa alianza kumchinja mbwa na kisha kumhifadhi ndani ya begi alililolitupa chumbani na kwamba siku alipokamatwa na wananchi na kupelekwa katika Kituo cha Polisi Nyamuswa, aliamriwa aondoke kijijini hapo kwa sababu kitendo alichokifanya hakikuwa cha kiungwana.

“Kwanza kabla ya kuua mtoto, mtu huyo alichinja mbwa na kumhifadhi ndani ya begi na kulitupia ndani. Wananchi walimkamata na kumpeleka Polisi na akaamriwa aondoke kijijini hapo kutokana na tabia hiyo mbaya,” alisema.

Alisema kuwa mtu huyo aliondoka kijijini hapo, lakini baadaye alirejea nyumbani hapo na kufanya mauaji ya mtoto huyo na kisha akatoroka. Aidha alisema kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa anafanya kazi ya kibarua cha ujenzi wa barabara inayojengwa kwa kiwango cha lami katika eneo hilo.

Katika tukio lingine mwanamume mmoja, Adamu Juma Kanyela (44) mkazi wa kijiji cha Salama Kati tarafa ya Chamriho wilayani hapa amemuua mke wake aitwaye Magiti Samwel (34) kwa kutumia fimbo. Alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 19, mwaka huu, alfajiri kijijini hapo na kwamba inadaiwa chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa mapenzi.
Ilielezwa kuwa, baada ya mauaji hayo wananchi wa kijiji hicho walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa na kumpeleka Polisi katika Kituo cha Nyamuswa. Polisi wilayani hapa imethibitisha matukio hayo.
Post a Comment
Powered by Blogger.