Waziri Luhaga Mpina Akitoza Faini Ya Mil. 10 Kiwanda Hiki.
NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi Ya Makamu Wa Rais,Muungano na Mazingira,Luhaga Mpina amekitaka
Kiwanda cha Nondo cha MMI Steel kilichopo maeneo ya Mikocheni kulipa faini ya Milioni 10 kwa kosa
la uchafuzi wa Mazingira na kukiuka sheria mbalimbali za usafi wa mazingira.

Ambapo kiwanda hicho kimetakiwa kulipa faini hiyo ndani ya Siku Saba pamoja na kurekebisha mifumo ya
utililishaji na kutoa Maji taka katika miundombinu yake ili isilete madhara kwa wananchi waliokuwa karibu na kiwanda hicho.

Agizo hilo lilitolewa  Dar es Salaam jana,wakati wa ziara yake ya kuangalia mazingira katika maeneo mbali mbali ya jiji,alisema kiwanda hicho kimekiuka sheria ya mwaka 2004 ya mazingira ya  kutililisha maji machafu katika maeneo ya wananchi ambapo ni kinyume cha sheria.

"Nimetoa adhabu hii ikiwa ni fundisho kwa viwanda vyote vinavyotililisha na kutoa ovyo maji taka kwani imekuwa ni hali ya kutisha kwa wananchi kupata magonjwa mbalimbali ikiwemo magonjwa ya
kipindupindu,"alisema  Mpina

Wakati huo huo Mpina,alitoa siku 17 kwa Shirika la Maji Safi na Maji Taka(DAWASCO) la Mkoa wa Dar es Salaam  na Pwani Kuhakikisha wanakomesha tatizo la utiririkaji wa maji taka yanayotoka viwandani
kiholela.

Alisema DAWASCO inatakiwa kutumia muda mfupi wa kutatua tatizo hilo kabla ya kuwaathiri wananchi
wanaozunguka maeneo yenye mitaro ya kupitishia maji hayo.

"Leo nimetembelea mtaa wa TPDC uliopo kinondoni kwa mara ya pili na kukuta tatizo la utililishaji wa maji ukiwa mbovu,hivyo nimetoa siku 17 ambazo najua DAWASCO itahakikisha inarekebisha miundombinu yake ili kulinda afya ya wananchi wa maeneo husika,"alisema

Kwa Upande wake Mwandisi wa DAWASCO,Erick Jackson alisema kuwa sababu zilizopelekea kuchelewa kumaliza tatizo la utililishaji wa maji taka katika mitaro ni uhaba wa vitendea kazi walivyokuwa navyo pamoja na baadhi ya miundombinu kutokuwa vizuri.

Alisema tayari wamewasiliana na uongozi wa Manispaa ya Kinondoni ili kuweza kupewa kibali cha kuchimba sehemu ya barabara ili kuweza kufanya marekebisho ya mabomba ya kutililishia maji ambayo
yamejaa mchanga.

Naye Ofisa Mazingira wa Manispaa ya Kinondoni,Mohammed Msangi alisema manispaa tayari imeshafikisha baadhi ya viwanda mahakamani vinavyokiuka sheria ya mazingira.

Akitaja viwanda hivyo ni pamoja na Kiwanda cha kuzalisha tiles cha Tembo,MMI steel pamoja na DAWASCO  kushindwa kufanya kazi zao kwa ufanisi na kwa wakati muafaka.
www.seetheafrica.com
Post a Comment
Powered by Blogger.