Serikali Imepata Suluhisho la Mazao Kwa Wakulima Limepatikana


 

PICS – KINGA DHIDI YA WADUDU WAHARIBIFU WA MAZAO

Nchi ya Tanzania ni mojawapo ya nchi inayozalisha mazao mengi kwa ajili ya biashara na pia mazao kwa ajili ya chakula ambapo wakulima wanatumia kila njia kupata nyongeza ya mazao shambani ili wanufaike zaidi.

Pamoja na jitihada za serikali za kuongeza uzalishaji wa mazao hapa nchini kutoka tani milioni 9.99 mwaka 2005/6 hadi tani milioni 16.01 mwaka 2014/15, upotevu wa mazao baada ya kuvuna nchini bado ni tatizo kubwa. Kwa mazao ya nafaka na mikunde inakadiriwa upotevu kwa mwaka ni asilimia 30 hadi 40.

Upotevu wa mazao husababisha nchi kutokuwa na uhakika wa chakula na kipato cha wakulima hupungua na hivyo huchangia pato la Taifa hushuka. Hata hivyo Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi imekuwa ikifanya jitihada za kupunguza upotevu wa mazao nchini kupitia program na mipango mbalimbali.

Serikali chini ya mpango wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa sasa (BRN) inakarabati na kujenga jumla ya ghala 275 katika wilaya 12 za Mikoa ya nyanda za juu kusini kwa ajili ya kuhifadhia zao la mahindi. Hivyo mradi huu wa mifuko ya PICS umekuja wakati muafaka katika kuchangia juhudi za serikali za kudhibiti upotevu wa mazao nchini. 


Chuo kikuu cha Purdue kwa kushirikiana na kiwanda cha Pee Pee Tanzania Limited (PPTL) kilichopo Tanga – Tanzania kimeleta teknolojia mpya “mifuko ya tabaka tatu” ijulikanayo kwa jina la PICS, mifuko iliyofanyiwa utafiti na wataalamu kutoka taasisi ya utafiti ya ukiliguru na chuo kikuu cha sokoine (SUA).


Utafiti uliofanywa na Profesa Rodes Makundi na Profesa Apia Masawe wa chuo kikuu cha kilimo (SUA) uliohusisha mifuko ya PICS umeonyesha sio tu mazao yatakuwa salama yakiwa ndani ya mifuko hiyo bali hata wadudu wanaobangua mahindi hufa baada ya siku kadhaa bada ya kukosa hewa na haitumii kemikali kabisa.
 

Wataalamu hao pia waliongeza kuwa mifuko hiyo yenye kisalfeti nje na mifuko miwili ya nailoni nzito, matumizi yake ni lazima mazao yawe yamekauka vizuri, ili kuzuia “wadudu wanaoharibu mazao kwa kunusa ikiwamo panya, lakini kwa sababu mfuko huo una nailoni mbili hawatapata harufu na waliokuwamo kwenye mazao kwa bahati mbaya hawatapata hewa kwa hiyo baada ya siku tano hadi saba watakufa.


Mifuko ya tabaka tatu ya PICS imetengenezwa mahsusi kwa teknolojia ya “hermetic” yaani isiyopitisha hewa, hivyo kuwanyima hewa ya oxygen wadudu ambao ni viumbe hai wanaohitaji hewa kuendelea kuishi. Mifuko miwili ya ndani isiyoingiza hewa na mmoja wan je wenye alama ya PICS – Purdue Improved crops storage.


Mifuko ya PICS imezinduliwa rasmi katika ukumbi wa bunge mnamo tarehe 13 June 2016 na Naibu spika wa bunge la Jamhuri wa muungano Mheshimiwa Dokta Ntulia Hudson na kuhudhuriwa na wabunge na mawaziri akiwemo waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mheshimiwa Charles Mwijage na Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa William Ole Nasha.


Mmoja wa wakulima mwenye ushahidi wa kutumia mifuko ya PICS, Akbarual Mshana ameeleza kuwa “mwezi wa nane 2014 nilihifadhi mahindi yangu bila kuyawekea dawa huku yakiwa na wadudu ndani kwenye mfuko mmoja wa PICS ili niweze kuthibitisha kama kweli hayatameng’enywa na nikaufungua mfuko mwezi wa tatu 2016, mahindi yalikuwa safi kabisa hata wale wadudu wote walikuwa wamekufa, hapo ndipo nikaamini kweli mifuko ya tabaka tatu ya PICS inasaidia kulinda mazao yangu” 


Mifuko ya PICS inatokana na kuwepo kwa wadudu waharibifu wanaoshambulia mazao ghalani na hasa dumuzi ambao huharibu mazao ya wakulima masikini katika nchi zinazoendelea. Teknolojia hii ilibuniwa katika miaka ya 1980 na Idara ya elimu ya wadudu (Entomology) ya Chuo Kikuu cha Purdue, kwa kushirikisha na wanafunzi, wafanyakazi na wadau kutoka Cameroon Kaskazini kwa msaada wa USAID. 


Mradi wa Mifuko ya PICs ililetwa nchini Tanzania mwezi Julai mwaka 2014 na Chuo Kikuu cha Purdue - Indiana, Marekani kwa kushirikiana na kiwanda cha PPTL kilichopo Tanga, ambacho kina uwezo wa kuzalisha mifuko 2,400,000 kwa mwaka. Toka Julai mwaka 2014 hadi Mei 2016 mifuko 470,000 imeshatengenezwa na kusambazwa katika maeneo mbalimbali nchini. 
www.seetheafrica.com 

Mifuko ya PICS ni teknolojia yenye ubora, rahisi kutumia katika ngazi ya kaya na pia hupunguza matumizi ya kemikali hivyo kuhakikisha usalama wa chakula. Huko Afrika Magharibi, teknolojia hii imeweza kutumika kwa takriban miaka tisa na baada ya mafanikio makubwa katika nchi hizo za Afrika Magharibi mradi huu umesambazwa katika nchi saba ambazo ni Malawi, Uganda, Ethiopia, Nigeria, Ghana, Burkina Faso na Tanzania. 


Mifuko hii imetengenezwa kwa ujazo wa kilogram 100 na inatumika kuhifadhi nafaka za aina zote kama vile mahindi, mtama, uwele, ulezi, ngano pamoja na mazao yote ya jamii ya mikunde.

Post a Comment
Powered by Blogger.