Obrey Chirwa Atimka Yanga .


AMISSI Tambwe akifahamu kuwa kuna uwezekano wa kupoteza namba katika kikosi cha kwanza baada ya ujio wa Mzambia, Obrey Chirwa, mshambuliaji huyo ameonekana kutokuwa tayari kukabiliana na hali hiyo baada ya kuonyesha makali zaidi katika ufungaji mabao.
Tambwe ameonyesha hali hiyo inayoashiria kugoma ‘kuchomeshwa mahindi’ na Chirwa, wakati ambao Mzambia huyo akiwa ametimkia kwao Zambia.
Ikumbukwe msimu uliopita Tambwe ambaye ni raia wa Burundi, ndiye aliyeibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kuifungia Yanga mabao 21.
Pamoja na mafanikio yake hayo, bado Yanga imeonekana kutoridhishwa naye na hivyo kumnasa Chirwa ili kucheza pamoja na Mzimbabwe mwenzake, Donald Ngoma.
Katika mchezo wake wa kwanza ndani ya kikosi cha Yanga dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Chirwa hakufanikiwa kufunga bao, lakini pia akionyesha kiwango cha kawaida tu.
Baada ya kuona kiwango cha Chirwa kupitia mchezo huo, inaonekana Tambwe amepata suluhisho la kuendelea kubaki katika kikosi cha kwanza ambalo si jingine bali kuongeza makali yake katika ufungaji mabao.
Katika mazoezi ya jana asubuhi yaliyofanyika Uwanja wa Boko Veterans nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, Tambwe alizidi kumweka njiapanda kocha wao, Hans van der Pluijm, katika kuamua ni nani wa kucheza pamoja na Ngoma kati ya Mrundi huyo na Chirwa, baada ya kufunga mabao matatu safiii.
Kwa bahati mbaya, amefunga mabao hayo wakati Chirwa akiwa amerejea kwao Zambia kuiaga rasmi familia yake baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Yanga.
Ni wazi iwapo Chirwa angekuwapo katika mazoezi ya jana na kuona cheche za Tambwe katika ufungaji, angefahamu kuwa ana kazi kubwa ya kupigania namba dhidi ya mkali huyo wa mabao ya vichwa na miguu.
Katika mazoezi hayo ya jana, mbali ya kufunga mabao hayo matatu akimtesa vilivyo kipa wao mahiri, Deogratius Munishi ‘Dida’, Tambwe alionyesha kiwango cha hali ya juu na kuwavutia mashabiki waliofika uwanjani hapo.
Tambwe alipangwa timu moja na nyota kadhaa wa Yanga kama Simon Msuva, Ngoma, Vincent Bossou, Said Makapu, Antony Matheo, Hassan Kessy, Juma Abdul  na Vicent Andrew ‘Dante’, wakati upande wa pili kulikuwa na Thaban Kamusoko, Kelvin Yondani, Haruna Ninyozima, Deus Kaseke, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Oscar Joshua, Pato Ngonyani na Mbuyu Twite.
Mbali ya Tambwe, mchezaji mwingine aliyeng’ara jana ni kiungo Kamusoko ambaye pamoja na kuonyesha utaalamu wake katika kumiliki mpira, pia alifunga mabao mawili kama ilivyokuwa kwa Matheo.
Kwenye mazoezi hayo, Pluijm alitumia muda mwingi kuwapa nafasi wachezaji wake kumiliki mipira na kushambulia ili kuwaweka fiti kuelekea mchezo unaofuata wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi dhidi ya Medeama ya Ghana.
Akizungumza baada ya mazoezi hayo, Pluijm alisema kuwa ana imani atafanya vema kwenye mchezo huo unaofuata kwani anawafahamu vema wapinzani wao.
“Nawajua Medeama na nimeshawahi kufanya kazi hata michezo yao miwili waliocheza niliiangalia hivyo najiandaa kwa ajili ya ushindani na kuibuka mshindi,” alisema.
Alipoulizwa juu ya kuondoka kwa Chirwa badala ya kujibu, Pluijm aligeuka kuwa mbogo na kuanza kutoa maneno makali kwa waandishi badala ya kujibu.
“Ulizeni maswali yanayojenga, kwanini maswali yenu yamekuwa ya kubomoa na kuuliza vitu ambavyo haviwahusu,” alisema kocha huyo.
Mmoja wa maofisa wa benchi la ufundi ambaye hakupenda jina lake kuandikwa gazetini, alisema: “Chirwa ameaga amerudi kwao kwa siku mbili lengo likiwa ni kuaga ila atarejea kuungana na wenzake hivi karibuni.”
Yanga na Medeama wanatarajia kukutana Julai 15, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, ukiwa ni mchezo wa raundi ya tatu.
Kikosi cha Pluijm kitalazimika kushinda mchezo huo ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kucheza nusu fainali ya michuano hiyo.
Mpaka sasa Yanga inashika mkia kwenye kundi hilo ikiwa imepoteza mechi zote mbili za kwanza, huku Medeama wakiwa na pointi moja baada ya kutoka suluhu na Mo Bejaia ya Algeria.

Source:Bingwa.
Post a Comment
Powered by Blogger.