Mjue Mtu Aliyedandia Helikopta Asafiri Kwa Ndege.

Swaleh Wanjala, Mkenya mwenye umri wa miaka 41 ambaye alidandia ndege magharibi mwa Kenya ametua mjini Nairobi lakini tofauti na safari yake ya awali, amewasili kama abiria rasmi ndani ya ndege baada ya Msamaria mwema kumlipia nauli akiandamana na mamake mzazi.
Swaleh alidandia ndege iliyokuwa imebeba mwili wa mfanyabiashara Jacob Juma mjini Bungoma mwezi mei mwaka huu.
Bwana huyo alidandia licha ya maafisa wa usalama kuwazuia watu waliowasili kuona maiti.
Mwanamume huyo ambaye amebandikwa jina la mwigizaji, James Bond, aliwasili jijini Nairobi leo akiwa na furaha baada ya kutua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta.
‘’Nimefurahi sana, nilihisi raha tofauti na kudandia ndege ambapo niliumia kutokana na upepo mkali angani,’’ alisema.
Jamaa huyo ambaye ni baba wa watoto wanne, ameongeza kuwa anajutia kitendo chake na kuwa hatowahi kurudia tena kosa hilo.
“Bado nahisi kuwa sijapata nafuu kabisa. Niliumia kwa sababu niliruka takriban mita kumi na moja kutoka hewani baada ya kushikilia ndege kwa muda.
Tofauti na safari yake ya awali juu ya ndege, ambapo alipanda kwa hiari wakati huu, ilikuwa vigumu kumshawishi Swaleh kusafiri kwa ndege.
“Nimeingiwa na woga tangu ajali hiyo, na sipendi tena ndege, alieleleza.
Bi Evelyne Namusya, mamake Swaleh waliosafiri naye hadi Nairobi, alieleza furaha ya kusafiri kupitia ndege akiwa na mwanawe.
"Hii ni mara yetu ya kwanza kusafiri kwa ndege na ninafuraha sana. Namshukuru mdhamini Joseph kwa kutuwezesha tufanikishe ndoto hii.”
Licha ya furaha aliyonayo, Bi Evelyne amesimulia kuwa alishangaa sana kwamba mwanawe alinusurika.
“Sikuamini kumwona akiwa hai. Sikutarajia kwa kweli,” alisema.
“Alivyofanya ni hatari na ni jambo la kushtua.”
Kwa upande wake, Mdhamini wa safari hiyo, Joseph Lendrix Waswa ambaye ni mfanyabiashara, ameeleza kuwa licha ya kulaumiwa kwa kufadhili safari hiyo, nia yake ni kuwaelemisha watu kama Swaleh juu ya hatari ya kusafiri njia bandia.
"Silengi tu kumfurahisha Swaleh, nia yangu ni kutoa funzo kuwa sio vizuri kuhatarisha maisha ikiwa kuna njia salama za kutimiza ndoto ya kusafiri kwa ndege,’’ alisema.
Mfanyabiashara huyo amesema kuwa anatarajia kumsaidia Swaleh Wanjala kuanzisha biashara ili ajimudu kimaisha na ajiepushe na vitendo vya kuhatarisha maisha yake.
Mbali na kumbandika jina Swaleh Wanjala, Wakenya wameanzisha mchezo wa kompyuta uitwao, ‘Bungoma hangman, unaowataka washindani kuonyesha uhodari wao wa kumzuia mchezaji wao hewani asiangushwe na lolote.
Kwa sasa Swaleh analenga kuendelea na maisha lakini hata hivyo, anasema bado anahisi maumivu.
“Bado sijapata nafuu, lakini nia yangu ni kuanzisha bishara na kuendeleza familia,’’ alimaliza.
Post a Comment
Powered by Blogger.