Mahakama ya Wilaya ya Ilala imemhukumu kwenda jela miaka 30, Gerlad Lucas(20) kondakta na mkazi wa Tabata Aroma Dar es Salaam baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa mali. Lucas anadaiwa kuiba vitu mbalimbali zikiwamo Laptop nne vyote vikiwa na thamani ya Sh milioni 96.7 mali ya kampuni ya Diamond Motors kinyume cha sheria. Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Catherine Kiyoja baada ya kujiridhisha na ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo na upande wa mashtaka ambao ulikuwa na mashaidi tisa. “Kulingana na ushahidi uliowasilishwa a upande wa mashtaka pasi kuacha shaka, ninakuhukumu kwenda jela miaka 30 baada ya kupatikana na hatia ya kuvunja na kuiba mali zenye zaidi ya Sh milioni 96.7 kinyume cha sheria, ili liwe fundisho kwa wote wenye tabia za wizi kama zako,” alisema Hakimu, Kiyoja. Wakili wa Serikali, Hilda Kato aliiambia mahakama hiyo kuwa hakukuwa na kumbukumbu za mashtaka ya nyuma dhidi ya mshtakiwa na hivyo kuiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa wote wenye tabia kama hizo. Katika utetezi wake juu ya kwanini wasipewe adhabu kali mtuhumiwa alidai kuwa anafamilia inayomtegemea pamoja na kaka yake ambaye ni mlemavu utetezi ambao ulitupiliwa mbali na mahakama hiyo. Kwa mujibu wa hati ya mashtaka ilielezwa kuwa katika tarehe isiyofahamika februari mwaka jana, mtuhumiwa akiwa na wenzake wawili ambao mmoja alifariki wakati kes hiyo ikiendelea huku wa pili akiachiwa huru. Walivunja na kuiba vitu hivyo kwenye barabara Nyerere ndani ya Manispaa ya Ilala vyote vikiwa na thamani ya Sh milioni 96.7 mali ya Diamond Motors.