Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA) lilikuwa limejiandaa kwenda mkoani Dodoma kwa ajili ya kuzuia mkutano Mkuu wa CCM uliopangwa kufanyika Julai 23 mwaka huu. Baraza hilo lilisema kuwa limeandaa zaidi ya vijana 4000 kwa ajili ya kusaidia na jeshi la polisi kuzuia mkutano huo. Leo mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe amezungumza na waandishi wa habari ambapo amewataka BAVICHA kusitisha zoezi hilo kwa kile alichoeleza kuwa wamegundua kuwa Jeshi la Polisi linaonyesha upendeleo kwa CCM. Amesema kuwa jana Julai 9 jeshi la polisi lilikuja na kauli ya kutatanisha baada ya kusema kuwa halikuwa limezuia vikao na mikutano ya kiutendaji ya vyama vya siasa hivyo mkutano mkuu wa CCM ni halali. Aidha Mbowe ametaka jeshi la polisi kuwaachi baadhi ya viongozi wa BAVICHA wanaoshikiliwa mkoani Dodoma na kuwa jeshi la polisi haliwezi kufanya kazi kwa upendeleo namna hii kwani linawazuia upinzani na kukipendelea chama cha siasa. Amesema licha ya vitimbwi vyote, upinzani utaendelea kutafuta njia mpya kuzungumza na wananchi hadi kitaeleweka.