ZIDANE KAMA NGARIBA HAOGOPI MKOJO.
Kelele kila kona. Tetesi kila mji. Anzia Turin nchini Italia, nenda Madrid nchini Hispania au geuka mjini Paris nchini Ufaransa utakutana na habari ileile. Ukitua Munich kule Ujerumani utasikia habari nyingi, angalau zimepoa kwa sasa.
Kwanini nasema hivyo? Kuna wakati Zidane anaudhi sana Haaaaaa! Hana muda na maongezi wala kujibu tetesi za usajili wa wachezaji wanaotakwa kwenda Real Madrid.
Nenda Juventus Turin utasikia Alvaro Morata anarudi nyumbani Santiago Bernabeu. Geukia jiji la Paris utasikia Mfaransa mwenzake, Paul Pogba anakuja Madrid.
Nenda mjini Bayern Munich utaiskia David Alaba anakuja Madrid. Si hao tu, nenda London Chelsea utasikia Eden Hazard anakuja Madrid.
Ukiingia kwa magwiji wa soka Brazil utasikia vita ya kumsajili Gabriel Jesus zimepamba moto kati ya Madrid na Barcelona.
Walioharibu zaidi ni Uingereza ambao wameamua kujitoa kwenye Jumuiya ya Ulaya na kusababisha baadhi ya wachezaji wasiokuwa na uraia wa Hispania (yaani hawajakaa miaka mitano Hispania) watakiwe kupunguzwa.
Utasikia Danilo, Bale au James ni lazima mmoja aondoke Madrid. Lakini mtu mmoja ambaye anaweza kutoa angalau kauli ya kuwatuliza mashabiki au kuwapa furaha ni Zinedine Zidane.
Zidane hana muda na dunia ya fununu. Hana muda na wale waandishi wanaomtafuta ili aseme chochote kuhusiana na tetesi hizo.
Utasikia Morata amefyatuka ooh! Sina cha kumthibitishia Zidane, mara hataki kuwa mshambuliaji chaguo la pili.
Ina maana Morata anatangaza vita na Karim Benzema kwamba yeye ndiyo aanze kisha Karim akae benchi.
Maneno yote hayo Zidane amekaa kimya. Hazungumzi chochote. Mara ya mwisho kumsikia Zidane akizungumzia wachezaji wapya au waliopo kuhusu maisha yao klabuni ni pale alipoulizwa kuhusu hatima ya Cristiano Ronaldo.
Zidane alisema hakuna nafasi ya kuondoka kwa mchezaji huyo. Hii ilituliza mashabiki na kuzima tetesi zote.
Lakini sasa Zidane amekuwa ngariba, haogopi mkojo (yaani kelele za kila kukicha juu ya nani anasajiliwa au nani anatakiwa kuanzia kikosi cha kwanza kati ya Benzema na Morata).
Kwanza Zidane alikwenda zake India. Kule alikuwa anaburudika maisha yasiyo ya soka kabisa. Alijitenga na dunia ya soka kwa kubarizi viunga vinavyozungumzia biashara zaidi kuliko maisha ya soka. Na hii ndiyo sura ya ukocha wa Madrid.
Kipindi cha nyuma nyakati za usajili makocha wetu walikuwa hawaishiwi kauli kwenye vyombo vya habari. Mara kwa mara ilikuwa unasikia kuwa kocha au rais amekuwa na pilika za kusajili ama kusema jambo fulani.
Madrid kwa sasa pametulia hapana habari  binafsi za kocha. Zidane ametimiza miaka 44 wiki hii lakini bado amekuwa mchoyo wa habari kwa vyombo vya habari.
Kitu kimoja unachotakiwa kukifahamu ni hiki. Wiki iliyopita aliyekuwa kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti, alipasua jipu kuwa Mratin Odegaard ulifanywa kwa minajili ya kukuza biashara na kuitangaza zaidi timu.
Alisema hakuwa mchezaji aliyepanga kumsajili lakini idara ya habari ya Real Madrid ilicheza na taarifa za kinda huyo kuonyesha kana kwamba alihitajika sana Madrid.
Sasa hebu jiulize, hadi waandishi wanamtafuta Carletto ina maana wanakaukiwa habari za kocha wa Real Madrid. Mwenyewe Zidane yuko kimya, hazungumzii chochote kuhusu mipango ya baadaye ya usajili.
Nafahamu kuwa dirisha la usajili bado kufunguliwa, lakini kwa kawaida kocha wa Real Madrid ni lazima awe na nyepesi nyepesi.
Chini ya Zidane hakuna hicho kitu. Presha yote ya kuiongoza Real Madrid ameimeza. Presha ya kocha kukabiliana na vyombo vya habari ametafuna na kuiona haina uwezo wa kuathiri chochote.
Kifupi Real Madrid imekuwa kimya na imetulia zaidi kuliko ilivyokuwa kawaida. Sasa basi hii ina maana Zidane haogopi ile dhana ya kocha kutozungumza. Kwamba kocha wa Madrid lazima awe mzungumzaji kidogo, lakini kwake hali imekuwa tofauti.

MPENI KAZI SANTIAGO SOLARI
Ni kweli kikosi cha Real Madrid Castilla hakijafanya vziuri msimu uliopita. Sasa mabosi wake wameamua kufanya mabadiliko kidogo. Jina linalotajwa zaidi ni Santiago Solari. Siku hizi uhendisamu wote umeisha. Hana madoido kama zamani, utu uzima umemjongelea.
Ujio wa Santiago Solari una maana ya kuleta akili mpya badala ya kuendelea na Luis Miguel Ramis aliyechukua mikoba ya Zidane. Nina sababu moja kubwa, Solari anaijua falsafa ya timu tangu akiwa na kikosi cha watoto.
Solari ameanzia Cadete B, Cadete A, Juvenil B na Juvenil A tangu alipowasili mwaka 2013 akiwa kama kocha. Nadhani huu ni wakati wake kuonyesha umahiri katika ukocha na akiwa mtu ambaye amecheza na Zidane kwa muda mrefu.
Faida ya hili jambo ni kushirikishana mipango yenye mwelekeo mmoja kuliko kuwa na falsafa mbili tofauti. Ina maana pia Solari atakuwa nguzo ya kuibua nyota wapya kama ambavyo Zidane alivyomtwisha jukumu zito la kupiga penalti kinda la Castilla, Lucas Vazquez.
Post a Comment
Powered by Blogger.