YANGA KUTUA MUDA WOWOTE JIJINI DAR HUKU CHIRWA KUIVAA TP MAZEMBE,TAMBE KUIKOSA.
Obrey Chirwa

MABINGWA wa soka Tanzania Bara, Yanga, wameondoka mjini Bejaia, Algeria jana kurejea Antalya, Uturuki ambapo wanatarajia kuunganisha ndege kurudi nyumbani kuendelea na kambi ya kujiandaa na mchezo wao wa pili wa Kundi A hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo, ambao mshambuliaji wao mpya, Obrey “Chola” Chirwa, anatarajiwa kucheza.
Yanga ilikuwa Algeria kwa ajili ya mchezo wao wa kwanza wa michuano hiyo uliopigwa juzi usiku dhidi ya Mo Bejaia ambapo wenyeji walishinda bao 1-0.
Pamoja na kufungwa, Yanga wameacha gumzo mjini Bejaia kutokana na kandanda la hali ya juu walilolionyesha kiasi cha kuwafanya wenyeji wao ‘kupaki basi’ kwa muda mrefu wa kipindi cha pili baada ya kupata bao lao pekee.
Na sasa akili zote za Yanga zimeelekezwa katika mchezo dhidi ya TP Mazembe utakaopigwa kati ya Juni 28 na 29, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wakiwa Dar es salaam, wachezaji wa Yanga wataendelea na mazoezi kabla ya kurejea nchini wiki ijayo tayari kuonyeshana kazi na Mazembe ambao juzi walianza vyema michuano hiyo kwa kuwafunga Medeama ya Ghana mabao 3-1.
Chirwa ambaye amesajiliwa hivi karibuni na Yanga akitokea klabu ya Platnum ya Zimbabwe, alishindwa kucheza mchezo wa juzi nchini Algeria kwani taratibu za uhamisho wake zilikuwa hazijakamilika.
Yanga watamkosa mshambuliaji wao Amis Tambwe kutokana na kuwa na kadi mbili za njano ambazo zitamfanya akose mchezo huu.
Kutokana na jitihada zinazofanywa na uongozi wa Yanga kwa ushirikiano na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lile la Zimbabwe na klabu yake ya Platnum, kila kitu kitakuwa kimekamilika kabla ya Juni 28.
Hivyo kuna uwezekano mkubwa kwa mshambuliaji huyo hatari kuungana na aliyekuwa pacha wake, Donald Ngoma, kuunda safu hatari ya ushambuliaji ya wakali hao wa Jangwani.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa Chola, beki wa kulia wa Yanga aliyetua Jangwani mwishoni mwa msimu uliopita akitokea Simba, atakuwa ‘ruksa’ kuichezea timu hiyo baada ya Juni 30, mwaka huu pale atakapokuwa amemaliza mkataba wake na klabu yake ya zamani.
Kessy alishindwa kuichezea Yanga katika mchezo wa juzi kwa kuwa bado ana mkataba na Simba, lakini angeruhusiwa kucheza iwapo tu Wekundu wa Msimbazi wangetoa kibali cha kumruhusu.
Lakini kwa kuwa hakuondoka vizuri Simba, Wekundu wa Msimbazi hao waliamua kumbania kwa kile kinachoonekana kukerwa na jinsi alivyowatenda kwa kusaini mkataba Yanga wakati ‘ndoa’ yake dhidi ya klabu hiyo ilikuwa haijavunjika rasmi.
Tayari jina la Kessy lipo Shirikisho la Soka Afrika (CAF) baada ya kutumwa na lile la Tanzania (TFF) hivyo kilichobaki ni kuhitimishwa kwa uhusiano wake na klabu yake ya zamani, yaani Simba.
Katika hatua nyingine, baada ya kuumia kwa beki wa kushoto, Oscar Joshua na Haji Mwinyi kuonyeshwa kadi nyekundu, Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm, anajipanga kuona ni vipi ataziba pengo lililopo katika nafasi hiyo.
Iwapo Joshua hatakuwa amepona hadi Yanga itakapovaana na TP Mazembe, Pluijm anaweza kumtumia Pato Ngonyani, kulia akiwapo Mbuyu Twite na katikati Kelvin Yondani na Vincent Bossou.
Lakini pia, Yondani anaweza kupangwa kushoto, kulia Twite, katikati Bossou na Nadir Haroub ‘Cannavaro’, huku kiungo mkabaji akiwa Thaban Kamusoko, kiungo mshambuliaji Haruna Niyonzima, winga wa kulia Simon Msuva, kushoto Deus Kaseke, wakati washambuliaji wa kati ni Ngoma na Chirwa.
Pia, Twite anaweza kupangwa kama beki wa kushoto, kulia Yondani au Pato, kulingana na kocha atakavyoona inafaa.
Katika kikosi cha Yanga kwa sasa, hakuna mchezaji mwenye uwezo wa kucheza namba zaidi ya tatu kama ilivyokuwa kwa Salum Telela aliyetemwa ambaye alizimudu vyema nafasi zote za nyuma kama beki wa kulia, kushoto, kati, kiungo, winga na hata mshambuliaji.
Post a Comment
Powered by Blogger.