WAARABU WAMEACHA KUTUDHARAU ILA TUMEBAKI TUNAJIDHARAU SISI WENYEWE.Yanga.

Miaka ya nyuma tulikuwa wasindikizaji katika michuano ya klabu bingwa Afrika lakini siku hizi Waarabu wameacha kutudharau. Wameanza kutuheshimu, wanatuchunguza na kuzifuatilia nyendo zetu kabla ya zile dakika 90 za uwanjani.
Lini waliwahi kufanya hivi? Kwanini wameanza kufanya hivi? Hakuna anayejua wala anayejisumbua kujua, tupo tumesimama na kushangaa shangaa kama walivyotuacha.
Waarabu si wajinga, wanajua nyakati zimebadilika na hakuna mdogo tena kwenye soka. Hawana sababu ya kuendelea kutudharau ikiwa wameshuhudia Brazil ikitolewa na Peru kwenye mashindano.
Kwanini watudharau? Wanapokosa majibu, huanza mara moja kuzicheza mechi zetu wiki moja au mbili kabla.
Bahati mbaya kwetu, tumeshindwa kuitafsiri hii heshima tuliyoanza kupewa na Waarabu na matokeo yake tumejisahau na kujikuta tukijidharau wenyewe.
Tunajidharau ndio. Mtu mwenye fikra timilifu hawezi kuendelea kusimama kila siku nakutamba hadharani kuwa ‘tumefungwa lakini cha moto wamekiona’. Huu ni umasikini wa fikra!
Mpaka lini tutaendelea kuwa masikini wa fikra? Unawakumbuka Etoile du Sahel? Mpaka dakika 90 za pambano lao na Yanga zinamalizika, wao waliondoka na sifa ya ushindi, vijana wa Jangwani wakaondoka na sifa ya kupiga pasi nyingi.
Nini kilitokea? Yanga iliyopiga pasi nyingi na kutawala mchezo kulekule Tunisia, ilirudi Bongo na kuendelea na Ligi ya Vodacom, Etoile tulioaminishwa kuwa ni wabovu wakaendelea na kubeba kombe la CAF.
Hatukumbuki haya? Nani katuroga Watanzania?
Hivyo hivyo ilivyokuwa kwa Etoile ya Tunisia, ndivyo ilivyokuwa dhidi ya Al Ahly ya Misri. Mara mbili Yanga imekuwa timu bora dhidi ya Al Ahly inayochezea kichapo baada ya dakika 90.
Tumewahi kujiuliza tunapokosea ni wapi? Wakati mwingine tunambebesha lawama Malaika wa bahati kwa upuuzi wetu wenyewe. Bahati haijawahi kushuka kwa asiyejiandaa kuipokea!
Tumebaki kusifiana ujinga na kujazana uchafu kwenye vichwa vyetu. Wanavyosifiana Yanga leo, ni kawa walivyosifiana Azam dhidi ya Esperance kipindi kile.
‘Bahati yao’ ndilo neno pendwa tunalolitumia kuficha aibu zetu. Tunajua tunapokosea? Hatujui na hatutakaa tujue kwa sababu tayari tumeshaamua kujidharau.
Kweli!? Katika karne hii bado tunasifiana kwa pasi na kumiliki mpira na kusahau kuwa kitu cha muhimu uwanjani ni ushindi! Hivi aliyeturoga alitumia uchawi wa nchi gani?
Lakini yote haya ni matunda ya kushindwa kuelewa kwanini Waarabu wameanza kutuheshimu. Ndio, kutuacha kutawala mchezo katika ardhi yao ni heshima kubwa wanatupatia.
Walishatufunga huku wakitukimbiza, sasa wanatufunga huku tukiwakimbiza. Walishatupiga sana 5-0 na sasa wametulia na kutupangia vipigo vya 2-1 au 1-0. Kwao kheri tu!
Si wajinga wale, wajinga ni sisi tunaoamini kutoka kufungwa 5-0 hadi 1-0 ni hatua nzuri kwenye maisha ya soka. Wametupumbaza eneo hilo, na kwa bahati mbaya zaidi, tumepumbazika.
Tangu Simba amfunge Zamalek pale Cairo, ni zaidi ya miaka 10 sasa imepita, hawajawahi kurudia hili kosa. Ni sisi ambao hatuoni kurudia kosa moja kila siku.
Tukianza kuelewa kwanini tumeanza kuheshimika, tutaanza kuelewa ni nini tunatakiwa kufanya. Hatutakiwi kuibeza heshima yao, tunatakiwa kuifanyia kazi kama wao wanavyozifanyia kazi dharau zetu.

Wengi wetu tukisikia Waarabu wanahaha kupata mikanda ya mechi za Yanga au Azam, huangusha kicheko na kudanganyana kwa nguvu ya akili za kishabiki kuwa, ‘Waarabu wameingia mchecheto’.
Klabu inayotoka kwenye taifa linaloongoza kwenye viwango vya soka Afrika, kukuchunguza ni kuingia mchecheto?
Tunaendeshwa kishabiki sana hata kwenye mambo ya msingi. Tunadharau mpaka yasio dharaulika. Wakati sisi tukitamba kuwa Waarabu wanahaha kutujua, sina hakika kama kuna mtu kwenye benchi la ufundi la Yanga alikuwa na mikanda ya Mo Bejaia.
Hatufungwi bahati mbaya. Tunajiandaa na hivi vipigo bila kujijua. Ngoja nikwambie kitu.
Binafsi sioni ajabu Yanga kuendelea kutawala soka dhidi ya timu za Kiarabu kwa miaka yote ambayo Hans Pluijm atakayokuwa na klabu hiyo. Unajua kwanini?
Chunguza michezo yote ya Yanga na timu za Kiarabu zinavyokuwa. Waarabu wameshajua ni ngumu sana kucheza soka la chini na timu yenye falsafa za Kiholanzi.
Si wao tu, nakuhakikishia, hata TP Mazembe watakuja kuutafuta mpira kwa tochi hapa taifa. Hili halijawa bahati mbaya, ubora wa Yanga umeundwa hapo.
Kuwadhibiti ni lazima watafute njia mbadala, lazima waje na mifumo tofauti ya kimchezo ili waweze kupata ushindi dhidi ya Yanga. Wanatulia na kushambulia kwa kushtukiza wakiwa na kasi sana.
Mpaka leo mashabiki wa Yanga wameingia kwenye mtego wa kuamini timu za Kiarabu huwa zinawafunga bahati mbaya tu. Wanaamini hivi nakusahau kuwa ni wao ndio huwa wanaingia kwenye mtego wanaotegewa.
Mfumo alioutumia Pluijm akicheza na Al Ahly kule Misri, ndio ule ule aliotumia kucheza dhidi ya Mo Bejaia kule Algeria. Kwanini wasipotee kwa staili ile ile?
Mwisho, benchi la ufundi la Yanga linabidi likae chini na kutengeneza hesabu nzuri za kucheza hizi mechi 6 za makundi. Hizi mechi huamuliwa zaidi kimbinu na si kiufundi.
Sikuona sababu ya Yanga kufungua uwanja ugenini ilihali pointi moja ingeweza kuwa na maana kubwa sana kwao kama wangeipata kwa kucheza kwa kujilinda.
Kuna mechi sita tu. Tatu nyumbani na tatu ugenini. Yeyote atakayeshinda tatu za nyumbani na sare moja ya ugenini, atafuzu bila ubishi.
Yeyote atayeshinda mechi mbili za nyumbani na sare moja nyumbani na moja ya ugenini atakuwa kwenye nafasi nzuri ya kupita. Kwanini Pluijm aliidharau pointi moja na kupanga kikosi chenye tamaa ya alama tatu ugenini?
Dhidi ya Al Ahly, Yanga walitakiwa kushambulia kupata bao kwa kuwa ule ulikuwa mchezo wa mtoano na tayari walishaharibu nyumbani, lakini dhidi ya Mo Bejaia, wamejichanganya wenyewe kwa kwenda na mawazo ya kushambulia.
Labda hayakuwa mawazo yake Pluijm, nguvu ya akili za kishabiki ilishamuingia na yeye akaamini kweli Mo Bejaia ni wabovu na anaweza kupata ushindi ugenini.
Tusipokubali kuacha ushabiki na kujiuliza kwanini wenzetu wanatuheshimu kwa kutuchunguza, tutaendelea kujidharau kila siku kwa kushangilia pasi huku tukiwa na kapu la magoli mkononi.
Post a Comment
Powered by Blogger.