UNAJUA HISTORIA YA DIMITRI PAYET? SOMA HAPA.

Dimitri Payet.

JUNI 10 mwaka huu, fainali za Kombe la Mataifa Ulaya (Euro 2016), zilianza rasmi nchini Ufaransa, zikishirikisha timu kutoka mataifa 24.
Mchezo wa ufunguzi ulikuwa kati ya Ufaransa na Romania ambapo wenyeji hao walishinda kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Stade de France.
Kabla ya mchezo huo, wakati wachezaji wakiwa wanapasha, nilikuwa nikimwangalia mno Dimitri Payet ambaye amekuwa akinivutia mno na uchezaji wake, lakini pia kisura nikimfananisha na kiungo wa zamani wa Manchester United, Mbrazil Anderson Oliveira, aliyekuwa akifahamika zaidi kwa jina moja la Anderson.
Wawili hao wamefanana kwa kiasi fulani, kuanzia sura hadi maumbo.

Kuzidi kujiridhisha zaidi kwa hilo, nilisogea katika kompyuta yangu na kuitafuta picha ya Anderson na kumlinganisha na Payet. Jamaa hawa wawili wamefanana hasa. Sijui kama hiyo ndiyo sababu inayonifanya nimpende Mfaransa huyo kama ambavyo nilikuwa nikivutiwa na uchezaji wa kiungo yule Mbrazil!

Hiyo inaweza kuwa moja ya sababu japo ukweli ni kwamba kati ya wachezaji wa Ligi Kuu England walioniteka msimu uliopita, Payet ni mmoja wao, wengine wakiwa ni Ng’olo Kante, Riyad Mahrez, Markus Rashford, Kevin De Bruyne Harry Kane, Graziano Pelle na wengineo wa viwango vyao.
Lakini hata Anderson hakuwa haba katika suala zima la kuuchezea mpira, alikuwa ni fundi ambaye kutemwa kwake Manchester United kuliniuma mno.
Baada ya mchezo kuanza Ijumaa iliyopita kati ya Ufaransa na Romania, nilitumia muda mwingi kuangalia uchezaji wa Payet kuliko hata ilivyokuwa kwa mastaa wengine wa Ufaransa kama Paul Pogba, Olivier Giroud, Antoine Griezmann na wengineo wa kiwango chao.
Ndani ya dakika 30 tu za kwanza, nilijiridhisha kuwa siku hiyo Payet angeibuka shujaa wa Ufaransa iwe ni kwa kufunga bao au kutoa pasi ya bao la kuamua matokeo ya mchezo.
Payet ambaye ni mchezaji wa kutegemewa wa klabu ya West Ham United ya Ligi Kuu England, alifanya kila alichojaliwa na Mwenyezi Mungu; kuanzia nguvu za kupambana, uwezo wa kuuchezea mpira atakavyo, kujiamini na kuufurahia mchezo wa soka.
Pia, siku ile Payet alionyesha uwezo wake alionao katika kumiliki mpira, kupiga chenga pamoja na pasi, lakini zaidi akicheza huku akifahamu kuwa Wafaransa zaidi ya milioni 66 wanamtupia macho yeye pamoja na wenzake, wakiwa wamebeba matumaini yao ya kulibakiza kombe kwenye ardhi yao.
Kama nilivyokuwa nikiamini, hatimaye Payet alipiga krosi kwa guu lake la kushoto kutoka wingi ya kulia, iliyozalisha bao la kwanza la timu yake, lililofungwa kwa kichwa na Giroud dakika ya 57.

Wakati wengi wakiamini mchezo ungeishia kwa sare ya bao 1-1, dakika ya 89 Payet alifanya kweli kwa kufunga bonge la bao akiwa umbali wa futi 25, pale alipoachia shuti la mguu ule ule wa kushoto uliotoa pasi ya bao la kwanza na kuipa nchi yake ushindi wa 2-1.
Bao hilo liliamsha shangwe miongoni mwa Wafaransa waliopo ndani ya nchi hiyo na kwingineko, lakini pia mashabiki wa mataifa mengineyo duniani kote, ikiwamo hapa Tanzania wanaoishabikia Ufaransa.
Baada ya kufanya mambo katika mchezo ule, wapo walioamini Payet angeendelea kukinukisha kwenye fainali hizo, japo kuna waliodhani huenda asing’are katika mechi zinazofuata.
Kwa upande wangu, kuelekea mchezo wao wa pili dhidi ya Albania juzi, kuna picha ilinijia akilini mwangu kuwa Payet angefunga bao dakika za lala salama wakati matokeo yakiwa 0-0.
Kama nilivyokuwa ‘nimeota’, ilikuwa hivyo pale mkali huyo alipofunga bao la pili la timu yake katika dakika za majeruhi, ikiwa ni baada ya Griezmann kufunga la kwanza dakika moja kabla ya filimbi ya mwisho.
Safari hii, Payet alifunga kwa mguu wake wa kulia, ikiwa ni baada ya kuwahadaa mabeki wawili wa Albania.
Kwa kiwango alichokionyesha kwenye mechi zote mbili za kwanza, ikiwa ni pamoja na mabao yake, jina la Payet limezidi kuwa maarufu kila pembe ya dunia.
Kila mpenzi wa soka anatamani kuona Payet akicheza, hata iwe kila siku. Nani anaweza kuthubutu kuikosa mechi ya Ufaransa ya Payet?
Ama kwa hakika Payet amezidi kuufanya mchezo wa soka upendwe zaidi kutokana na kile anachokifanya uwanjani na ni wazi soko lake litakuwa juu baada ya fainali hizo za Ufaransa.

Dimitri Payet ni nani?

Ni kijana aliyezaliwa Machi 29, 1987 kwa sasa akiwa na umri wa miaka 29, akikipiga kama straika ndani ya klabu ya West Ham United na ni mmoja wa nyota wa kutegemewa wa timu ya Taifa Ufaransa.
Payet anayetajwa kubarikiwa kuwa na uwezo mkubwa wa kukokota mpira na ufundi wa hali ya juu katika mchezo huo, inaelezwa kuwa historia yake katika soka ni ya kipekee.

Kama ilivyo kwa wanasoka wengi hapa nchini Tanzania na kwingineko, Payet alianza kucheza soka akiwa na umri mdogo ambapo kipaji chake kilizidi kushamiri kadiri alivyokuwa akikua.
Lakini miaka 11 iliyopita, alikatishwa tamaa na kocha wake wa timu ya Le Havre ya Ufaransa pale alipoambiwa kuwa hana mwonekano wa kisoka na pia amekosa hamasa ya mchezo, hivyo kuamua kurejea nyumbani kwao katika Kisiwa cha Reunion.

Baada ya kucheza Ligi Kuu ya Reunion kwa takribani miaka miwili akiwa na kikosi cha AS
Excelsior, akiwa mbele ya watazamaji 2,000-3,000, alionyesha kiwango cha hali ya juu hivyo kuwafanya maskaunti wa klabu ya Nantes iliyokuwa Ligi Kuu ya Ufaransa, Ligue 1, kumtaka.


Pamoja na kuambiwa ana kipaji cha soka, aligoma kwenda kujiunga na Nantes hali iliyomfanya kujibishana na baba yake, Alain pamoja na mjomba wake, Jean-Marc waliomtaka kutopoteza fursa hiyo.
Baba na mjomba huyo, walimshauri kijana wao huyo wakati huo akiwa na umri wa miaka 17, kutopeteza nafasi hiyo ya kwenda kucheza soka la kulipwa Ulaya na ndipo alipokubaliana nao, lakini baada ya majibishano ya muda mrefu kidogo.

Payet alisema juu ya hilo: “Nilidhani ndoto yangu ilikuwa imeyeyuka. Sikutaka kusikia au kuzungumzia juu ya mimi kurejea tena Ufaransa.
“Nilivunjwa moyo na uamuzi wa kutemwa. Nilihisi sikuwa katika kiwango cha juu.
“Lakini nafasi ya pili ilipokuja niligombana na baba na mjomba, lakini walinishawishi kwamba ningejaribu bahati yangu kwa mara nyingine.

“Nilitumia miaka minne nikiwa Le Havre na waliponiambia hawatakuwa tayari kuwa nami, kwasababu sikuwa vema kwa ligi daraja la pili, hili lilinivunja moyo sana.

“Niliamua kubaki katika kisiwa changu na kucheza soka huko.
“Baada ya Le Havre, nilikuwa mchezaji mdogo kuliko wote katika ligi ya Reunion. Nilianza kucheza nikiwa na umri wa miaka 16. Hapo ndipo nilipoonwa na watu wa Nantes.”

Payet anasema: “Niliporejea nyumbani kutoka Le Havre, familia yangu ilifanya kila kitu kunifanya nijisikie vizuri. Walisema: ‘Ok, mambo hayakwenda vema lakini angalau umejaribu’.
“Walisema wananikaribisha kwa moyo mmoja kuishi nyumbani kama niliamua hivyo.
“Lakini ofa ya Nantes ya kunirejesha Ufaransa ilipokuja, niliikubali kwasababu ya kumridhisha baba yangu, kwa wakati huo.
“Anapenda sana soka na alikuwa hajapata nafasi ya kutoka nje ya Reunion.
“Niliamua kukabiliana na changamoto zaidi kwa sababu yake na kuwa na jambo hilo kichwani mwangu, kulinisaidia sana nilipokuwa Nantes.”
Ukiachana na klabu hizo mbili, Payet pia alipitia klabu za Saint-Etienne, Lille na Marseille kabla ya Slaven Bilic kumnasa kwa dau la pauni milioni 10 kipindi cha kiangazi mwaka jana na kumfikisha West Ham.

Tangu alipotua England, kiwango chake kimezidi kukua akiwa ametengeneza nafasi za mabao zaidi ya 80 msimu uliomalizika Mei mwaka huu, zikiwa ni pasi 35 za mabao zaidi ya alivyofanya nyota wa Barcelona, Lionel Messi.
Ni kutokana na makali yake hayo, haikushangaza pale West Ham ‘walipomfunga pingu’ zaidi kwa kumpa mkataba mpya wenye thamani ya mshahara wa pauni 120,000 kwa wiki.

Ndani ya West Ham, Payet amekuwa mchezaji wa kipekee na ndio maana wakali hao wa Upton Park wanamlinganisha na mkongwe wa klabu hiyo, Paolo Di Canio.
Juu ya ubora wake huo, Payet anasema umechangiwa na mshambuliaji wa zamani wa Ufaransa, Jean-Pierre Papin ambaye baadaye alishuka na kucheza katika nafasi zote tatu nyuma ya mshambuliaji wa mbele.

Lakini baada ya hapo, Payet alijikuta ‘akioza’ kwa nyota wa zamani wa Brazil, Ronaldinho aliyekuwa akimkubali mno kutokana na utaalamu wake katika kuuchezea mpira.
Payet alisema: “Watu wanasema alipenda kuwanyanyasa mabeki lakini siku zote alipatia kwa kila alichokifanya. Sababu ya kumpenda ni kutokana na uwezo wake wa kuburudisha kwa soka lake maridadi, lakini pia kuisaidia timu yake kushinda.

“Bado ninachukulia soka kama mchezo hata kama wapo wanaofikiria vingine, hasa wanaouona mchezo huo kwa mtazamo wa kiuchumi.
“Nimekuwa nikijaribu kutoa burudani uwanjani kwani mashabiki wamekuja ili kupewa burudani kwa soka la kuvutia.”
Tayari mashabiki wa West Ham wameanza ‘uchokozi’ kwa kuimba kuwa Payet ni “bora zaidi ya Zidane”, jambo linalomchekesha Payet.
“Hayo yanaweza kuwa maoni ya mashabiki, lakini nikiwa kama mtu niliyemwona Zidane akicheza mara nyingi, siwezi kusema mimi ni bora zaidi yake!”
Hata hivyo, Payet amekiri kuwa England imechangia kwa kisi kikubwa kukuwa kwa kiwango chake akisema: “Nilikaribishwa vizuri mno na makocha,
wachezaji wenzangu na mashabiki.

“Tuwe tunacheza nyumbani au ugenini, nimekuwa nikionyeshwa upendo wa hali ya juu na mashabiki.
“Sikutarajia kama mambo yangekuwa kama ilivyokuwa.”
Kwa upande mwingine, familia ya mwanasoka huyo kwa sasa bila shaka itakuwa katika kilele cha furaha kutokana na mafanikio ya ndugu yao huyo.
Lakini pia, mke wake, Ludivine na watoto wake, Noa na Milan ambao wamekuwa wakifika uwanjani kumshuhudia akicheza, ni wazi watakuwa wenye kujisikia fahari kubwa kuwa na mtu kama Payet.

Alikuwa muuza ‘mitumba’
Pamoja na jina lake kutamba kila kona ya dunia, Payet amepitia maisha ambayo baadhi ya mastaa wa mataifa mbalimbali na wa hapa nchini, wawe ni wanasoka au wasanii, nao wameyaonja.
Wakati akiwa katika kikosi cha timu ya vijana ya FC Nantes, Payet alikuwa akifanya kazi katika duka la nguo.
Alifanya hivyo ili kumwezesha kupata fedha za kujikimu akiwa kama mtoto wa kiume kama ambavyo tumekuwa tukiambiwa hata mkali wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’, alipitia maisha hayo, lakini kwa sasa akiwa matawi ya juu.
Na sasa wakati nyota ya Payet ikiwa inang’ara kwenye fainali hizo za Euro, wengi wamekuwa wakijiuliza iwapo mkali huyo ataendelea kuwa ‘mkombozi’ wa Ufaransa na hatimaye kutwaa ubingwa wa michuano hiyo?
Bila shaka, hilo ni jambo la kusubiri na kuona kama si kusikia, lakini mwisho wa siku, Payet anaufanya mchezo wa soka uzidi kupendwa kutokana na utaalamu wake ndani ya uwanja.
Post a Comment
Powered by Blogger.