TP MAZEMBE JEURI KUMSAJILI MCHEZAJI HUYU WA YANGA KWA GHARAMA YOYOTE.


MOJA ya kauli zilizotolewa na TP Mazembe walivyotua Tanzania kupambana na Yanga, ni kuwa mbali na mechi hiyo pia walipanga kuondoka na wachezaji wenye vipaji kutoka Tanzania kama walivyofanya kwa Mbwana Samatta.
Na baada ya mechi hiyo ya juzi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuibuka na ushindi wa bao 1-0, jina la winga mpya wa Yanga, Juma Mahadhi, ndilo lilinasa kwenye akili za mashabiki na mabosi wa Mazembe kama ilivyokuwa kwa Samatta mwaka 2011.
Kwa sababu uwezo ulioonyeshwa juzi na Mahadhi ambaye alikuwa anacheza mechi yake ya kwanza akiwa na jezi za Yanga, umewashawishi mashabiki na viongozi wa Mazembe kubeba jina la kinda huyo na kupania kulipeleka kwa tajiri wa klabu hiyo, Moise Katumbi.
Inafahamika kuwa Katumbi anawakubali na kuwaamini sana mashabiki wake na siku zote wakimpa jina la mchezaji huwa tayari kuvunja benki kumsajili kama alivyofanya kwa Samatta miaka mitano iliyopita.
Katika mchezo wa juzi licha ya ugeni wake katika mechi kubwa za kimataifa, Mahadhi alionyesha kiwango cha hali ya juu na kuwakuna watu waliojitokeza kushuhudia pambano hilo na wengi wao wakaishia kusema tu kuwa kijana huyo hatadumu Jangwani kwa sababu watu watafika bei.
Kwa upande wake kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm, alionekana kukoshwa na kiwango cha kinda huyo na kummwagia sifa kemkem baada ya pambano hilo la pili kwa Yanga katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
“Nimefurahishwa na kiwango chake (Mahadhi), huu ni mchezo wake wa kwanza, lakini ameonyesha vitu vya hali ya juu uwanjani najivunia kuwa naye katika kikosi change,” alisema Pluijm.
Aliongeza licha ya Uwanja wa Taifa kufurika mashabiki kibao lakini Mahadh alionyesha ukomavu wa hali ya juu na kuupiga mpira mwingi huku akiiweka katika wakati mgumu ngome ya TP Mazembe.
Mahadhi alionekana kuwa na kasi na kutengeneza kona mbili ambazo hata hivyo hazikuzaa matunda kwenye mchezo huo ambao Yanga walilala kwa bao 1-0.
Hata hivyo, katika dakika 65, Mahadhi aliumia na kushindwa kuendelea na pambano hilo na nafasi yake kuchukuliwa na Geofrey Mwashiuya.
Post a Comment
Powered by Blogger.