TAZAMA MIUJIZA MINNE YA OBREY CHIRWA ALIYOKUJA NAYO YANGA.

OBREY Chirwa aliyesajiliwa na Yanga hivi karibuni, ametua Jangwani na miujiza minne iwapo atakuwa makini inaweza kumsaidia kung’ara katika mchezo wao wa Jumanne ya wiki ijayo wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Mchezo huo utakaochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ni wa pili baada ya awali Yanga kuvaana na Mo Bejaia ya Algeria na kupokea kipigo cha bao 1-0 katika mchezo ambao Wanajangwani hao walicheza ugenini.

Ikiwa ni siku chache baada ya kusajiliwa na Yanga, Chirwa amekuwa akipewa naafsi kubwa kung’ara akiwa na kikosi hicho kinachonolewa na Mholanzi, Hans van der Pluijm, kutokana na ukweli kwamba hatakuwa mgeni mbele ya nyota wa timu hiyo, Thaban Kamusoko na Donald Ngoma aliowahi kucheza nao FC Platinum ya Zimbabwe.

Muujiza wa kwanza wa Chirwa alioingia nao Yanga unaoweza kuibeba Yanga kuichapa kirahisi TP Mazembe ni ukweli kwamba atakuwa uwanjani kuichezea timu yake hiyo huku mwamuzi wa kati akiwa ni Mzambia mwenzake, Janny Sikazwe, ambaye ni wazi hatakuwa tayari kuona ‘ndugu’ yake huyo akitoka kapa uwanjani katika mchezo wake wa kwanza.

Hii ni bahati ya mtende kwa mchezaji kucheza mchezo wa kwanza wa kimataifa wa timu yako mpya huku mwamuzi akitoka nchini kwao ambaye anaweza kuwasiliana naye kisirisiri wakati mchezo unaendelea kuona ni vipi anakuwa upande wa Yanga.

Chirwa anaweza kufanya kila linalowezekana kusaka bao japo la kuotea na kama atashindwa, anaweza kujipenyeza hadi ndani ya 18 na kujenga mazingira ya kufanyiwa madhambi au kuguswa na mabeki wa TP Mazembe hali inayoweza kumfanya mwamuzi huyo kumpa penalti.

Muujiza mwingine wa Chirwa unatokana na TP Mazembe ambapo straika huyo atawavaa wababe hao wa DRC wakati wakiwa katika majonzi baada ya bosi wao, Moise Katumbi, kuhukumiwa kufungwa jela miaka mitatu kutokana na kukutwa na hatia ya kununua nyumba kinyume cha sheria kwenye mji ulio Mashariki mwa Lubumbashi.

Bila shaka, hiyo ni fursa ya pekee kwa Chirwa kutumia mwanya huo kufanya kweli Jumanne ili kuwashawishi wapenzi wa Yanga kwamba hawajapotea njia kumsajili.

Muujiza wa tatu ni kitendo cha Chirwa kujikuta akiwa hana mpinzani katika nafasi ya mshambuliaji wa kati wa kucheza pamoja na Ngoma kutokana na aliyekuwa ‘pacha’ wa Mzimbabwe huyo, Amissi Tambwe, kutumikia adhabu ya kadi za njano alizoonyeshwa kwenye mechi zilizopita za michuano hiyo.

Mbali ya miujiza hiyo, mwingine uliombeba Chirwa na kujikuta akiwa katika kikosi cha kwanza cha Yanga ni rekodi ya Tambwe kwenye michuano ya kimataifa ambapo amekuwa akishindwa kung’ara kama inavyokuwa katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Tangu ametua katika Ligi Kuu Bara, Tambwe ameibuka mfungaji bora mara mbili, lakini kwenye mechi za kimataifa, amekuwa akishindwa kutamba hali inayofungua milango kwa Chirwa kupewa nafasi ya kuona kama anaweza kufurukuta.

Kwa mwenendo wa Tambwe katika mechi za kimataifa, hata kama asingekuwa anatumikia adhabu ya kadi za njano, ni wazi Pluijm angempa nafasi Chirwa kuona iwapo anaweza kuongeza lolote kwenye akaunti yao ya mabao ya ngazi hiyo.

Na sasa kinachosubiriwa na wapenzi wa Yanga ni kuona iwapo Chirwa anaweza kuongeza makali katika safu yao ya ushambuliaji, akishirikiana na Ngoma.
Chirwa, imeelezwa kuwa ametua Yanga baada ya kuvutiwa na dau nono la mabingwa hao wa Tanzania Bara ambapo anatarajiwa kuvuna Dola za Marekani 168,000 (sh milioni 363.476) kama mshahara katika kipindi cha miaka miwili atakachokaa Jangwani kwa mujibu wa mkataba aliosaini.

SEETHEAFRICA.COM  limedokezwa kuwa kwa mwezi Chirwa atakuwa akilipwa Dola 7,000 (sh milioni 15.14), kitita ambacho kimewashtua mashabiki wa soka wa Zimbabwe anakotoka mshambuliaji huyo na tayari inaelezwa kuwa wachezaji kibao wa huko wanatamani kuja Tanzania kucheza soka la kulipwa.

Chirwa mwenye umri wa miaka 22, anatajwa kuwa na uwezo wa hali ya juu kiasi cha kutabiriwa kufanya vema ndani ya kikosi cha Pluijm kama ilivyokuwa kwa Ngoma na Kamusoko.

Mbali ya Sikazwe, waamuzi wasaidizi wake Jumanne watakuwa ni Jarson Emiliano dos Santos kutoka Angola na Berhe O’Michael wa Eritrea, wakati Wellington Kaoma wa Zambia atakuwa mwamuzi wa akiba, huku kamishna akiwa ni Celestin Ntangungira wa Rwanda.
Post a Comment
Powered by Blogger.