TAZAMA HAPA E-MAIL YA NSAJIGWA INA SIRI NZITO YA TP MAZEMBE NA MADEAMA.BAADA ya kuitazama TP Mazembe wakati ikiichapa Medeama ya Ghana kwa mabao 3-1 kwenye mchezo wa Kundi A la Kombe la Shirikisho Afrika, nahodha wa zamani wa Yanga, Shedrack Nsajigwa, tayari ameandaa ripoti kamili na kuituma fasta Uturuki kwa Hans van der Pluijm, ili aitumie kujua siri za miamba hiyo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

 Wakati Yanga ikiwa Algeria ikivaana na Mo Bejaia katika mchezo ambao walipoteza kwa kufungwa bao 1-0, kocha wa vijana wa timu hiyo, Nsajigwa alikuwa nchini DRC akiichunguza TP Mazembe wakati ilipokutana na Medeama jijini Lubumbashi.

Yanga walijua fika kuwa baada ya mechi ya Mo Bejaia walitakiwa kukutuna na Mazembe kwenye Uwanja wa Taifa, Juni 29 mwaka huu na ndiyo maana wakaamua kumtumia Nsajigwa kuwasoma wapinzani wao hao ili waweze kujua ni namna gani wanaweza kuwachapa Taifa.

Baada ya kurudi nchini, Nsajigwa aliandaa ripoti kamili ya ubora na udhaifu wa TP Mazembe kwa siri kubwa na kuituma fasta Uturuki kwa Pluijm na benchi lake la ufundi akitumia njia ya barua pepe (e-mail) ili kufanikisha mauaji ya timu hiyo ambayo anachezea Mtanzania, Thomas Ulimwengu.

Akizungumza na Seetheafrica.com , Nsajigwa alisema tayari amekabidhi ripoti yake kwa benchi la ufundi la Yanga kwa njia ya mtandao na anawaachia walimu wa timu hiyo kuifanyia kazi ripoti yake anayodai kuwa imeshiba vya kutosha.

“Ni kweli nilikuwa Congo na tayari nimerudi na kuandaa ripoti ambayo ambayo itabaki kuwa siri yangu na klabu.” Alisema Nsajigwa. “Kwa kuwa tupo vitani na kama ujuavyo tuna mchezo mgumu dhidi ya Mazembe kwa hiyo si kila kitu lazima tuweke wazi.”

Nahodha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, alisema kuwa alitumia juzi na jana kuandaa ripoti hiyo ambayo jana mchana aliituma Uturuki kwa barua pepe na kupokelewa kwa furaha na Pluijm ambaye jioni ya jana alianza kuifanyia kazi.

Nsajigwa alisema amekabidhi kwa benchi la ufundi la Yanga ripoti kamili iliyoshiba kuhusiana na wapinzani hao wa Yanga ikiwa ni pamoja na aina ya soka wanalocheza.

“Nimekabidhi ripoti iliyokamilika subiri ifanyiwe kazi uone lakini siwezi kuzungumzia kile nilichokiandika ila wewe amini uwezo wa kuwafunga Mazembe tunao kutokana na kikosi tulichonacho,” aliongeza Nsajigwa.

Licha ya Nsajigwa kugoma kufunguka kile alichokiweka kwenye ripoti hiyo, wachambuzi mbalimbali wa soka nchini wanadai kuwa kikubwa ambacho kinaweza kuwa kwenye ripoti hiyo ni wachezaji wa kuchungwa wa TP Mazembe, ubora na udhaifu wao na juu ya mfumo gani unaweza kuwaua Taifa.
Post a Comment
Powered by Blogger.