NGOMA NA TAMBWE WAZICHAPA KAVUKAVU KISA CHIRWA.
WAKATI wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika wakiwa kwenye maandalizi ya mwisho ya mchezo wao wa pili hatua ya makundi dhidi ya TP Mazembe ya Congo, inadaiwa kuwa mastarika wake wa kimataifa, Amissi Tambwe (Burundi) na Donald Ngoma (Zimbabwe), wametofautiana na kusababisha wawili hao kuzichapa kavukavu.

Tukio hilo linaloonekana huenda likajenga uhasama baina ya wachezaji hao, lilitokea Ijumaa iliyopita wakati wakiwa kwenye mazoezi ya mwisho nchini Uturuki walikokuwa wameweka kambi ya wiki mbili kabla ya kurejea nyumbani kuwavaa Mazembe hapo kesho.
Kwa mujibu wa mmoja wa watu aliyeshuhudia wakati wawili hao wakizichapa kuwa jambo hilo lilitokea baada ya Ngoma kufunga bao lililoonekana ni la kuotea na kocha Hans Van Pluijm  kutopiga filimbi kuashiria kuwa bao hilo ni la kuotea wakati awali  Tambwe alifunga bao kama hilo na kocha alipiga  filimbi kuashiria  Mrundi huyo aliotea.

“Hakuna mtu ambaye aliwaza kama wawili hao wangeweza kukunjana na hatimaye kupigana. Ilikuwa kama kawaida ya kocha aliweka timu A na B,  wakati wakiendelea kucheza  golini akiwa Ally Mustapha ‘Barthez’ , Tambwe alifunga bao ambalo kocha lilikataa  akidai lilikuwa la kuotea na muda mfupi, Ngoma naye akafunga kama lile la kwanza lakini kocha hakupiga  filimbi.

“Ndipo Tambwe na wachezaji wengine walipomweleza Ngoma kuwa halikuwa bao halali, cha ajabu Ngoma alimfuata Tambwe na kumwambia kwanini aseme hivyo wakati hata yeye anapendelewa na kocha mara nyingi, lakini pia  Ngoma alimweleza Tambwe kuwa muda wake wa kukaa benchi umefika kwani mchezaji mpya Mzambia, Obrey Chirwa ni mzuri  zaidi yake,” alisema mtoa habari huyo na kuongeza:

“Baada ya kuambiwa hiyo, Tambwe alimjibu Ngoma kuwa kila mmoja ataonyesha uwezo wake uwanjani, lakini ghafla Ngoma akamvaa Tambwe na kuanza kumshushia kipigo jambo lililowalazimu wachezaji na viongozi kuingilia kati suala hilo kipindi ambacho tayari Tambwe alishaumia.”

Mtoa habari huyo aliongeza kuwa ilimlazimu daktari kumpa huduma ya kwanza Tambwe na baadaye akapelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu zaidi huku baadhi ya wachezaji sita akiwemo Ngoma wakirejea Jumamosi huku Tambwe akirejea Tanzania jana.
Post a Comment
Powered by Blogger.