RAIS MAGUFULI ATAKA POLISI KUJIONGEZA.

Rais John Magufuli amewataka polisi kujiongeza katika utendaji kazi wao bila kusubiri majambazi kufikia hatua ya kuwanyang’anya silaha katika vituo au kuvamia nyumba, watu na kuwanyang’anya mali zao.Aidha, alisema umefikia wakati wa polisi sasa kugangamala na kutosita kuwanyang’anya majambazi silaha haraka na akiwataka kutumia mbinu za medani kwani wananchi wamechoka kutafuta mali zao huku watu wengine wakija kuchukua na kuahidi kuangalia namna ya kuwanunulia helikopta kwa ajili ya doria.Magufuli alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizindua mpango wa usalama wa raia katika kuboresha utendaji kazi kwa kutumia Mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) awamu ya pili unaoanza kutekelezwa katika wilaya ya Kinondoni Julai mosi mwaka huu na baadaye kusambaa nchi nzima baada ya miaka mitatu na kupunguza uhalifu kwa asilimia 10 kila mwaka. Uzinduzi huo pia ulihudhuriwa na Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete na Katibu Mkuu Kiongozi John Kijazi. “Naomba niwe mkweli na muwazi kwa sababu sitaki kuwa mnafiki kwani yapo mambo yalikuwa yakinikereketa na kuniudhi unapoona jambazi anavamia kituo cha Polisi na kuua polisi kisha kuondoka na silaha au anakwenda kuiba mahali na ana silaha anaondoka hivi hivi hili limekuwa linanipa wasiwasi kidogo.“Kama mnazo bunduki za kutosha kwa nini jambazi aondoke bila kunyang’aywa silaha anayotumia haraka haraka ,ninaposema haraka haraka mnanielewa, kwa nini jambazi aende mahali akafanye ujambazi na polisi mshindwe kumnyang’anya silaha yake haraka haraka,” alihoji.
Post a Comment
Powered by Blogger.