Harun Niyonzima Atoa Maneno Mazito Dhidi Ya Mo Bejaia.

Kiungo wa Yanga Harun Niyonzima.
KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Haruna Niyonzima, ameweka wazi kuwa licha ya kwamba mchezo wao dhidi ya Mo Bejaia ya Algeria utakuwa mgumu, lakini watahakikisha wanapata matokeo mazuri.

Wanajangwani hao watashuka dimbani mwishoni mwa wiki hii ugenini kucheza na Waarabu hao mchezo wa Kombe la Shirikisho barani Afrika hatua ya makundi.

Kutokana na umuhimu wa michuano hiyo, Yanga wameamua kutimkia nchini Uturuki kujichimbia huko wakichukua mazoezi ya nguvu chini ya kocha wao mkuu, Hans Van de Pluijm, lengo kubwa likiwa kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.

Niyonzima ambaye amepachikwa jina la ‘fundi’ na mashabiki wa kikosi hicho kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuchezea mpira, amesema wao kama wachezaji watapambana kuhakikisha hawadondoshi pointi yoyote.

“Kwa ujumla hii michuano ni migumu sana kwani tunakutana na timu mbalimbali zenye uwezo tofauti, hilo tunalitambua na tumejipanga kupambana kwa kila hali kuhakikisha tunaifikisha Yanga mahala pazuri,” alisema.

Yanga wapo kundi A katika michuano hiyo sambamba na Mo Bejaia, Medeama ya Ghana pamoja na waliokuwa mabingwa watetezi wa Ligi ya mabingwa barani Afrika, TP Mazembe ya Congo.
Post a Comment
Powered by Blogger.